July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM yaonyesha ubunifu wa kemia kutatua changamoto mbalimbali

Na Joyce Kasiki

IDARA ya Kemia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imetambulisha teknolojia mbalimbali bunifu zinazolenga kutoa suluhisho katika sekta za ujenzi, nishati na mazingira kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumza katika maonesho hayo Juali Mosi mwaka huu, Mhadhiri wa Chuo hicho  , Jasson  Kajage, alisema wamewasilisha teknolojia ya lami baridi  inayotumia madini ya Duraman, ambayo huongeza uimara wa barabara na kupunguza athari za maji na chumvi zinazosababisha mashimo na uharibifu wa miundombinu.

Anesema tofauti na lami ya kawaida, teknolojia hiyo haihitaji kupashwa moto wala kufunga barabara kwa muda mrefu, kwani barabara inaweza kuanza kutumika ndani ya saa mbili hadi tatu baada ya ujenzi.

Kajage amesema pia wamebuni bidhaa ya Novasem, aina ya saruji inayotumika kutengeneza matofali mepesi na matofali yenye uwezo wa kuzuia joto na baridi kuingia ndani ya majengo, hatua inayosaidia kupunguza matumizi ya viyoyozi na feni pamoja na gharama za nishati.

Aidha, amesema wameunda teknolojia ya kusafisha gesi ya biogas kwa kuondoa harufu na uchafu, hatua inayowezesha gesi hiyo kuwaka kwa mwali wa buluu na kuweka msingi wa kuihifadhi kwenye mitungi kwa matumizi ya majumbani.

Kwa upande wa sekta ya uchimbaji, amesema wamezalisha bidhaa ya Bentox, inayotengenezwa kwa malighafi za ndani na kutumika kuimarisha kuta za visima wakati wa uchimbaji, hivyo kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza usalama wa kazi.

Kajage amewataka wananchi kutembelea banda la Idara ya Kemia katika maonesho ya Sabasaba ili kujionea teknolojia hizo, huku akibainisha kuwa wanaendelea kutoa mafunzo kwa mafundi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha ubunifu huo unatumika kwa ufanisi nchini.