Na Joyce Kasiki
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewahimiza wakulima nchini kutumia miche bora ya parachichi iliyoboreshwa ili kuongeza uzalishaji na kipato, huku ikitoa elimu kuhusu teknolojia za kisasa katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika banda la TARI, mtafiti kutoka TARI Kifyulilo, mkoani Iringa, Moses Mkumbo alisema taasisi hiyo imeleta aina tatu za parachichi ambazo ni Hass, Fuerte na Kikulu, kila moja ikiwa na sifa zinazokidhi mahitaji tofauti ya soko.
Alieleza kuwa parachichi aina ya Hass ndiyo inayolimwa zaidi kwa biashara na kusafirishwa nje ya nchi kutokana na ganda lake gumu linalowezesha kudumu hadi siku 28 baada ya kuvunwa endapo litahifadhiwa katika mazingira yanayofaa. Aidha, aina hiyo ina kiwango kikubwa cha mafuta kinachoifanya ipendwe zaidi katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wa aina ya Fuerte, alisema inaweza kudumu hadi siku 14 ikiwa imehifadhiwa vizuri, huku aina ya Kikulu ikiwa na uwezo wa kudumu hadi siku saba katika mazingira bora ya uhifadhi.
Mtafiti huyo alisema, mbali na kutoa elimu kwa wakulima, TARI pia huzalisha miche iliyoboreshwa kwa teknolojia ya kuunganisha miche (grafting), inayopunguza muda wa mti kuanza kuzaa kutoka miaka mitano au sita hadi miaka miwili na nusu au mitatu.
Alifafanua kuwa teknolojia hiyo huwasaidia wakulima kuanza kuvuna mapema na hivyo kuongeza kipato kwa muda mfupi, jambo ambalo limeongeza mahitaji ya miche hiyo miongoni mwa wakulima mbalimbali nchini.
Alisema mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa, jambo linalodhihirishwa na ongezeko la mahitaji ya miche inayozalishwa na TARI.
Aidha, aliwataka wananchi na wakulima kupata miche kutoka katika vituo rasmi vya TARI ili kuhakikisha wanapata miche bora yenye ubora unaokubalika.
Alitaja vituo vinavyopatikana miche hiyo kuwa ni TARI Kifyulilo (Iringa), TARI Uyole (Mbeya), TARI Tengeru (Arusha) na TARI Maruku (Bukoba).
Alihitimisha kwa kuwahimiza wakulima kuchangamkia fursa ya kilimo cha parachichi kutokana na ongezeko la mahitaji ya zao hilo ndani na nje ya Tanzania, akisema lina mchango mkubwa katika kuongeza kipato na kukuza uchumi wa kaya.
Amewaasa wananchi kufika banda la TARI kujionea teknolojia mbalimbali za uzalishaji na kujipatia elimu ya miche bora itakayowasaidia katika uzalishaji wa mazao mbalimbali shambani itakayowasaidia kujiinua kiuchumi.

More Stories
TIRA yazindua rasmi Kijiji cha Bima Sabasaba
TCPM yatoa elimu kuhusu faida za nguzo za zege
Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi