



Na Mwandishi wetu,Dodoma
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imehitimisha zoezi la utoaji wa huduma kwa wananchi katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo takribani wananchi 1,400 walinufaika na huduma mbalimbali zinazohusu sekta ya ardhi.
Akizungumza Julai 1, 2026 kuhusu mafanikio ya zoezi hilo, Afisa Ardhi Mteule wa Mkoa wa Dodoma, Letare Shoo, amesema huduma hizo zilitolewa kuanzia kipindi cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Juni 16 hadi 23, 2026, na kuendelea hadi Juni 30 kufuatia maelekezo ya Serikali.
Ameeleza kuwa uamuzi wa kuendelea kutoa huduma ulitokana na maelekezo yaliyotolewa na Mgeni Rasmi wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yalifanyika katika Viwanja vya Chinangali Park kuanzia Juni 16 hadi 23, ambapo taasisi mbalimbali za umma zilitoa huduma kwa wananchi.
Wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi aliielekeza Wizara ya Ardhi kuendelea kutoa huduma hadi Juni 30, 2026 ili kuwapa wananchi wengi zaidi fursa ya kupata huduma za sekta ya ardhi.
Shoo amesema utekelezaji wa maelekezo hayo umewezesha wananchi wengi kupata huduma za ushauri, ufafanuzi wa masuala ya ardhi pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Wizara.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuharakisha maendeleo ya Taifa.

More Stories
TIRA yazindua rasmi Kijiji cha Bima Sabasaba
TCPM yatoa elimu kuhusu faida za nguzo za zege
Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi