April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pre-Betika Tulia Marathon kuhamasisha mazoezi kwa jamii

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

TAASISI ya Tulia Trust kupitia Mbeya Jogging Club imeandaa mbio za pamoja zijulikanazo kama Pre-Betika Mbeya Tulia Marathon, zitakazofanyika Aprili 25, 2026, kwa lengo la kuhamasisha mazoezi na kukuza michezo katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 23, 2026, Mratibu wa Michezo kutoka Taasisi ya Tulia Trust, Lugano Mwangosi, amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya maandalizi ya mbio kubwa ya Betika Mbeya Tulia Marathon, ambayo mwaka huu inaadhimisha msimu wake wa kumi.

Amesema mbio hizo kuu zinatarajiwa kufanyika Mei 15 hadi 16 katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Mwangosi ameeleza kuwa Pre-Betika Mbeya Tulia Marathon imeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kumtambulisha mdhamini mkuu pamoja na kutoa hamasa kwa jamii kushiriki mbio hizo, ikiwa ni pamoja na kuendeleza utamaduni wa mazoezi ya pamoja mwishoni mwa mwezi.

“Mbio hizi zitakuwa za taratibu, zikianzia maeneo ya Kabwe, Mafiati, Sangu, Sinde, Ujenzi na Iyunga (Lift Valley), na kuhitimishwa Uwanja wa Sokoine, ambapo kutakuwa na michezo mbalimbali ya uwanjani,” amesema Mwangosi.

Ameongeza kuwa michezo hiyo ni pamoja na mbio za mita 100, kukimbia na gunia, kuruka kwa urefu (Long Jump), pamoja na mashindano ya kukimbia huku mshiriki akiwa amebeba yai kwenye kijiko.

Kwa upande wake, Mratibu wa Pre-Betika Mbeya Tulia Marathon, Lwiza John, amesema maandalizi yanaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa michezo ya watoto pia imepewa kipaumbele ili kuibua vipaji vipya vya riadha vitakavyoweza kuiwakilisha nchi kimataifa.

Ametolea mfano mafanikio ya mwanariadha nyota Alphonce Simbu katika mashindano ya Boston Marathon, akisema ni kielelezo cha umuhimu wa kuendeleza vipaji tangu ngazi ya chini.

Naye Mwenyekiti wa Tulia Trust Mbeya Jogging Club, Gabriel Mwaisanila, amesema vilabu vya jogging vina utaratibu wa kuandaa mbio za pamoja kila mwisho wa mwezi, na kwamba tukio hilo la Aprili ni maalum zaidi kutokana na maandalizi ya marathon hiyo kubwa.

“Amehimiza wananchi wa Mkoa wa Mbeya na maeneo ya jirani, ikiwemo Mbalizi, kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizi, kwani mbali na afya, pia ni fursa ya kushiriki michezo mbalimbali,” amesema.