April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari sita  wapata ajali wakitoka kambi ya matibabu  

*Ni baada ya dereva kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka barabarani 

*Wawili wameruhusiwa,wanne wanaendelea na matibabu

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

MADAKTARI sita wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa  Mwanza Sekou-Toure, wamejeruhiwa  kufuatia ajali ya gari waliyokuwa wakisafiria wakitokea kambi ya matibabu ya kibingwa katika hospitali ya Icheja, Wilaya ya Kwimba mkoani humo.

Ajali hiyo ilitokea Machi 27, 2026 majira ya saa 12:30 jioni katika barabara ya Jojiro,kitongoji na kijiji cha Maremve, Kata ya Igongwa, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,akizungumza Machi 28,2026 jijini hapa,amesema ajali hiyo ilihusisha gari namba T.231 AWT aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop lililokuwa likiendeshwa na Dkt.James Nkya (38), mkazi wa Lumala-Pasiansi, Wilaya ya Ilemela.

Ambapo ameeleza kuwa madaktari hao walikuwa njiani kurejea Mwanza mjini baada ya kutoa huduma za kibingwa,katika hospitali ya Icheja wilayani  Kwimba, walipofika eneo la tukio kijiji cha Maremve,  dereva alijaribu kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka katikati ya barabara ya vumbi. 

Kutokana na hali hiyo, gari  liliacha  barabara na kugonga gema na kisha kupinduka na kusababisha majeruhi kwa madaktari hao.

Katika ajali hiyo, madaktari sita walipata majeraha na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu. Majeruhi hao ni Dkt. James Nkya (38) na Dkt. Self Mmka (38), wote wakazi wa Wilaya ya Ilemela, waliolazwa katika Hospitali ya Sekou-Toure.

Wengine ni Dkt. Stanley Makundi (37), mkazi wa Mahina na Dkt. Avetha Masawe (35), mkazi wa Buswelu, waliolazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Madaktari wengine waliopata majeraha ni Dkt. Mary Urasa (27), mkazi wa Ngudu, Wilaya ya Kwimba pamoja na Dkt. Frank Mgeta (42), mkazi wa Nyamh’ongolo, Wilaya ya Ilemela, ambao wote wametibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuimarika.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa majeruhi wanne wanaendelea na matibabu huku wawili wakiwa tayari wameruhusiwa,chanzo cha ajali ni dereva wa gari kujaribu kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka katikati ya barabara hiyo ya vumbi.

Aidha,ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.