
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya
MAMLAKA ya Usimami i wa Bandari Ziwa Nyasa imewataka wafanyabiashara na wananchi kuitumia bandari hiyo katika usafirishaji wa mizigo na kuondoa dhana ya kujenga hofu kuhusu usalama wa mizigo yao na kueleza kuwa Bandari hiyo ipo salama.
Akizungumza Octoba 23, 2026 wakati wa Maonesho ya Biashara na Uwekezaji ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Ziwa Nyasa (TPA), Thomas Kusaga, amesema wameshiriki maonesho hayo kutangaza huduma za bandari hiyo pamoja na kuwapa elimu wananchi na wafanyabiashara na wadau.
Amesema bandari hiyo inafungua fursa nyingi kwa wafanyabiashara kutokana na kuhudumia pia nchi jirani za Msumbiji na Malawi.
“Hivyo tunaamini kupitia fursa hii wananchi wanaweza kupata vitu vipya hasa kwenye biashara na kilimo, ambacho asilimia kubwa ya wananchi wanategemea,” amesema Kusaga.
Amefafanua kuwa kazi kuu ya mamlaka hiyo ni kupakia na kupakua mizigo katika ukanda wa Nyasa kwa kushirikiana na nchi za Malawi na Msumbiji.

Amesema miongoni mwa mizigo inayohudumiwa ni pamoja na makaa ya mawe na mizigo ya kawaida inayopitia bandari ya Mbambabay iliyopo Mkoani Ruvuma.
Amesisitiza kuwa bandari hiyo ni salama zaidi kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo kwenda maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Biashara na Uwekezaji ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Ibrahimu Mangula, amesema lengo la maonesho hayo ni kuvutia wawekezaji kuwekeza katika mikoa hiyo.
Mangula amesema maonesho hayo pia yanatoa fursa za ajira za muda mfupi kwa vijana, ikiwemo kazi za usafi, ujenzi wa mabanda na ulinzi.
“Naamini hii itawasaidia wafanyabiashara kubadilishana uzoefu na kufahamu mwelekeo halisi wa shughuli zao pamoja na kupata uzoefu mpana zaidi,” amesema.
Naye mfanyabiashara Juma Maulid, aliyeshiriki maonesho hayo, amesema amejifunza huduma nyingi za Mamlaka ya Bandari ambazo hakuwa akizifahamu awali.
“Nilikuwa naamini kusafirisha mizigo kwa magari pekee ndiyo njia sahihi, kumbe ipo Bandari ya Ziwa Nyasa ambayo inasafirisha mizigo kwa usalama zaidi. Maonesho haya yametufungua wengi kibiashara,” amesema Maulid.

More Stories
Madiwani wawataka wazazi kuchangia chakula mashuleni
Tanzania yaimarisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kupelekea 2030
Bima ya Afya kwa Wote kunufaisha 57,129