
Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
WAZAZI na walezi Jijini Mbeya wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchangia chakula mashuleni ili kuwawezesha watoto kusoma kwa utulivu, kuongeza bidii katika masomo na kupunguza utoro.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Mbeya, Farida Ngoyi wakati madiwani hao walipotembelea Shule ya Msingi Iganjo na kukabidhi msaada wa chakula kwa wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mpango wao wa kusaidia shule mbalimbali katika Majimbo ya Mbeya Mjini na Uyole.
Ngoyi amesema baadhi ya wazazi katika Shule ya Msingi Iganjo wamekuwa wakisita kuchangia chakula, hali inayowalazimu wadau kujitokeza kusaidia mahitaji ya wanafunzi.

“Mkuu wa shule, tunakupa pole kutokana na changamoto ya wazazi kutoshiriki kikamilifu katika kuchangia chakula. Inaonekana wazazi wa Shule ya Msingi Iganjo bado wanahitaji kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao,” amesema.
Ameongeza kuwa madiwani hao, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Benki ya CRDB, wameweza kupata msaada wa chakula kwa ajili ya wanafunzi hao.
Aidha, Ngoyi amewataka wazazi na walezi kutambua kuwa chakula shuleni ni sehemu muhimu ya kuwawezesha watoto kushiriki kikamilifu katika masomo, akieleza kuwa wanafunzi wanapopata chakula wanaweza kuendelea na masomo kwa utulivu na kupunguza uwezekano wa kutoka shuleni bila ruhusa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Madiwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Mbeya,Mh. Atu Msai, amewapongeza madiwani wenzake kwa moyo wa kujitolea na kutenga muda wao kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni.
“Tuendelee kuwa na moyo huu wa kujitolea. Tumekuja kukabidhi magunia matatu ya chakula kwa ajili ya watoto wetu wa Shule ya Msingi Iganjo. Madiwani hawa wataendelea kutembelea kata hii ya Igawilo na kuona namna wanavyoweza kusaidia shule nyingine kulingana na uwezo wao,” amesema Msai.
Naye Gladnes Erick, mwanafunzi wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi Iganjo, amewashukuru madiwani hao kwa msaada huo wa chakula na kutoa wito kwa wazazi kuendelea kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi wapate fursa ya kuendelea na masomo badala ya kukosa masomo kutokana na changamoto zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Mbeya, Magret Kalonga, amewapongeza wanafunzi wa shule hiyo kwa kuonyesha utulivu na nidhamu, akieleza kuwa juhudi za kuhakikisha wanapata chakula shuleni zinalenga pia kuhamasisha wazazi na walezi kushiriki katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.


More Stories
Tanzania yaimarisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kupelekea 2030
Bima ya Afya kwa Wote kunufaisha 57,129
TMA: El Niño kuathiri mvua za msimu 2026 -2027