April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kushughulikia changamoto za CHAKUHAWATA

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

MKURUGENZI Msaidizi wa Masuala ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais, Mwanaamani Juma Mtoo, amesema Serikali inatambua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na imejipanga kushughulikia changamoto zinazowakabili ili kuboresha mazingira ya kazi.

Mtoo amesema hayo jijini hapa leo Machi 28,2026 wakati akifungua Kikao cha Kamati Tendaji ya Taifa ya Chama Cha Kutetea na Kulinda Haki za Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA)kilichokutana kujadili masuala mbalimbali yanayokihusu chama hicho.

Amesema hayo baada ya kusikiliza changamoto za wanachama hao ambapo amesema hatua mbalimbali tayari zinaendelea kuchukuliwa kushughulikia changamoto hizo na kusisitiza kuwa uwepo wa changamoto ni sehemu ya mchakato wa maendeleo.

“Tunatambua mchango wa vyama vya wafanyakazi katika kulinda haki za watumishi. Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi,” amesema Mtoo.

Akitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wanachama wa CHAKUHAWATA Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Abisias Lutandika,amesema kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa haziishirikishi CHAKUWAHATA katika mabaraza ya wafanyakazi, jambo linalowanyima wanachama wake uwakilishi muhimu katika maamuzi ya kikazi.

Changamoto nyingine ni pamoja na kuwahamisha walimu viongozi wa chama bila sababu za msingi, kucheleweshwa kwa stahiki zao za uhamisho, pamoja na kuwepo kwa makato ya vyama viwili kwenye mishahara ya baadhi ya wanachama kinyume cha sheria.

Pia, chama hicho kimeeleza kusikitishwa na baadhi ya wanachama wake kutoshirikishwa katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), huku wengine wakidai hata kuondolewa kwenye maandamano wanapojitokeza kushiriki.

Katika mapendekezo yao, CHAKUWAHATA imeiomba Serikali kuingiza vyama vya wafanyakazi katika mfumo wa kielektroniki wa utumishi (ESS) ili kurahisisha mchakato wa kujiunga au kujiondoa kwenye vyama bila kuingiliwa na waajiri.