April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni Bendera ya upendo yamfikia Mwagama,aomba bajaji

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

MKAZI wa Kata ya Iganjo, Mtaa wa Shinga jijini Mbeya, Enelrst Mwagama, ambaye ni mlemavu wa miguu na baba wa familia yenye watoto sita, amemwomba Spika Mstaafu wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, kumsaidia chombo cha usafiri aina ya bajaji ili kujikwamua kiuchumi.

Mwagama amesema anaishi katika mazingira magumu kutokana na changamoto ya ugonjwa wa kisukari unaomsumbua kwa muda mrefu, hali inayomfanya kushindwa kutembea kwa urahisi na hivyo kushindwa kujipatia kipato cha kuendesha maisha yake pamoja na familia.

“Wakati mwingine hali yangu ya afya inakuwa mbaya kiasi kwamba siwezi hata kutembea bila kutembea siwezi kufanya kazi, na bila kazi hakuna chakula kwa ajili yangu na watoto wangu,” amesema Mwagama.

Ameeleza kuwa licha ya kujishughulisha na ushonaji wa viatu, bado hana wateja wa kutosha kumwezesha kupata kipato cha uhakika. Kwa sasa, anasema kipato chake cha siku ni kati ya Sh3,000 hadi Sh6,000, kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji ya familia yake pamoja na gharama za matibabu.

Mwagama ameongeza kuwa sehemu ya kipato hicho hutumika kununua dawa za kisukari, ambapo hulazimika kutenga kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 kila siku ili kuendelea na matibabu.

Akizungumza Machi 27, 2026 wakati wa kampeni ya Bendera ya Upendo iliyofika Mtaa wa shinga, Kata ya Iganjo, Mwagama amesema msaada unaotolewa na Dkt. Tulia kwa makundi ya watu wenye uhitaji, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Pasaka, ni kitendo cha ibada na upendo wa hali ya juu.

“Ninamshukuru sana Dkt. Tulia kwa msaada wa chakula aliotupatia. Hii ni faraja kubwa kwangu na familia yangu. Lakini nikiweza kupata bajaji itanisaidia kujitegemea zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, mkazi wa eneo hilo, Dotto Mwasake, amesema ujio wa msaada huo umeleta matumaini mapya kwa familia ya Mwagama pamoja na wananchi wengine wenye uhitaji katika eneo hilo.

Amesema licha ya changamoto wanazokumbana nazo, hatua ya Dkt. Tulia kuwafikia watu wenye ulemavu, wazee na makundi maalum katika mitaa yote 61 ya kata 13 za Jimbo la Uyole ni ya kupongezwa.

“Huyu ana watoto sita, maisha si rahisi. Wanahitaji kula, kusoma na kupata mahitaji muhimu. Kitendo cha kuwafikia ni jambo kubwa sana na la kuigwa,” amesema Mwasake.

Dkt. Tulia kupitia kampeni yake ya Bendera ya Upendo ameendelea kugusa maisha ya watu mbalimbali wenye uhitaji, akiwemo walemavu na wazee, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusaidia makundi yaliyo hatarini.