April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi Ilemela wahimizwa chanjo ya polio

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

IKIWA imesalia siku moja kukamilika kwa zoezi la utoaji chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10,kupitia kampeni inayofanyika kwa mikoa saba ikiwemo ya Kanda ya Ziwa,wazazi wilayani Ilemela wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo.

Akizungumza Machi 25,2026,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,Amiri Mkalipa wakati akizindua zoezi la chanjo ya polio (nOpV2) ambapo kiwilaya uzinduzi huo umefanyika katika kituo cha Afya Buzuruga,amesema chanjo ya polio inatolewa ili watoto waweze kuwa na afya pamoja na kukabiliana na maradhi.

Mkalipa amesema,polio ni ugonjwa mbaya unaoweza kusababisha ulemavu kwa watoto huku akiwasisitiza kuachana na dhana potofu kwamba mtoto akichanjwa atapoteza nguvu.

“Usimsababishie mtoto ulemavu kwa kutompa chanjo ya polio, tuachane na dhana potofu kuwa mtoto akichanjwa atapoteza nguvu na ataumwa, mtoto aliyechanjwa ndio anapata afya,”amesema Mkalipa.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Sarah Ng’hwani amewaomba wazazi waliofika kituoni hapo kuwa mabalozi kwa kuwaeleza wenzao umuhimu wake kwa watoto ili wahamasike kuwatoa watoto wao wapatiwe chanjo hiyo.kwani kinga ni bora kuliko tiba.

Kwa upande wake mmoja wa wazazi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo, Raymuna Lemah ametoa wito kwa wazazi ambao watoto wao hawajapata chanjo wahakikishe wanapata kwani haina madhara yoyote bali kuwakinga na maradhi mbalimbali na huduma hiyo inatolewa bure bila gharama yoyote.

Mratibu wa chanjo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Shamte Almas,amesema kampeni hiyo ya utoaji chanjo ya polio katika mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani imeanza Machi 24 na inatarajia kukamilika Machi 27/,2026.

Ikiwa ni awamu ya kwanza ya kampeni hiyo ambapo kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jumla ya watoto 146,956 walio chini ya umri wa miaka 10 wanatarajiwa kupatiwa huduma hiyo ya chanjo.