April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja la Gagi kumaliza adha ya usafiri

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Shinyanga

MRADI wa ujenzi wa daraja la zege la Gagi katika Kata ya Ndembezi, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,linatarajiwa kuondoa adha ya usafiri iliyokuwa inawakabili wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani kwa muda mrefu.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 11.2 na upana wa mita 8.2 linajengwa katika barabara ya Gagi inayounganisha Kata za Ndembezi na Ngokolo, na linatarajiwa kuboresha mawasiliano na shughuli za kijamii na kiuchumi katika manispaa hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Diwani wa Kata ya Ndembezi ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,Upendo Sawa,amesema kukosekana kwa daraja hilo kwa muda mrefu kulisababisha mateso kwa wananchi, hususani kipindi cha masika.

Ameeleza kuwa kabla ya ujenzi huo, eneo hilo lilikuwa halipitiki kirahisi baada ya kivuko cha awali kusombwa na maji, hali iliyosababisha wanafunzi kushindwa kufika shule kwa wakati, na wakati mwingine kuvushwa kwa malipo huku wajawazito wakikumbana na hatari kubwa.

“Changamoto ilikuwa kubwa,Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na wajumbe wake walikuwa wanakaa hapa kusubiri kuwavusha watoto,lakini kwa sasa wananchi wana kila sababu ya kufurahia mradi huu ambao umeleta matumaini mapya,”amesema Sawa.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samson Pamphili, amesema daraja hilo linajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 105.4,kupitia Mfuko wa Dharura (CERC) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia,unaolenga kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mafuriko.

“Wakati wa masika eneo hilo lilikuwa halipitiki kutokana na mafuriko makubwa ambayo yalisababishwa na mvua,hivyo tumelipa kipaumbele kwenye mipango yetu kwa kujenga daraja kupitia chanzo chochote cha fedha,”amesema Mhandisi Pamphili.

Amebainisha kuwa mradi huo ulianza Desemba 29, 2025 na unatarajiwa kukamilika Juni 28, 2026, lakini hadi sasa umefikia asilimia 93 ya utekelezaji na unatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Machi 28, 2026.

“Muda wa ujenzi wa daraja hili ni miezi sita.Lakini ujenzi wake umefanyika kwa haraka na ifikapo Machi 28, 2026 litaanza kutumika,”.

Mkazi wa mtaa wa Botengwa, Emmanuel Exavery Hanya,amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, eneo hilo lilikuwa hatari kupitika hasa wakati wa mvua, jambo lililowaathiri zaidi wanafunzi, wajawazito na wafanyabiashara.