March 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge ya Miundombinu yaipongeza TTCL,Kituo cha ukusanyaji wa data kwa utendaji kazi wake

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi za Maendeleo kwenye Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.Huku amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali umesaidia kuanza kutengeneza faida ya sh. bilioni 17 katika Shirika la Mawasiliano (TTCL) ambapo awali lilikuwa likijiendesha kihasara.

Akizungumza hayo jana wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea Kituo cha ukusanyaji wa data cha Taifa kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, Kakoso amesema miaka ya nyuma wizara hiyo ilikuwa ikipata fedha kidogo lakini kwa sasa wameshuhudia mambo mengi yaliyofanywa na Serikali katika wizara hiyo.

Amesema miaka ya nyuma TTCL ilikuwa likijiendesha kwa hasara lakini wamepata taarifa amnauo kwa sasa imeanza kutengeneza faida kubwa.”Tunaimani kwamba Serikali ikiendelea kuwasimamia watafika mahala ambapo ni pazuri watakuwa na utengenezaji wa faida,”amesema.

Mwenyekiti Kakoso amesema katika kituo hicho cha ukusanyaji data, kinaumuhimu mkubwa kwa taifa hasa katika sekta ya mawasiliano.”Bila ya kituo hiki shughuli zote za mawasiliano zitasimama hasa zile zinazohusiana na mawasiliano ikiwa pamoja na ukusanyaji wa mapato,”amesema.

Akizungumzia changamoto,Mwenyekiti Kakoso amesema wameishauri Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukifanyia ukarabati kutuo hicho.”Zikitoka fedha kiasi cha sh.bilioni 70 kituo hicho kitakuwa kizuri na cha kisasa kwa sababu miundombinu yote chakavu itakuwa imebadilishwa,”amesema.

Mwenyekiti Kakosa amemuomba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki asimamie kupata fedha hiyo kwa lengo la kukarabati vyema mitambo hiyo.

Akizungumzia kwa upande wa TTCL amesema wameiomba Serikali waendelee kusimamia wafanyakazi wa shirika hilo kutoka katika dhana ya kutegemea ruzuku na badala yake wajikite katika kubuni bishara mbalimbali.”Mheshimiwa Waziri naamini ukiwasimamia vyema wakipata kibali watajiendesha na faida .

Kwa upande wake Waziri ,Angela Kairuki, ameiishukuru kamati hiyo kutembelea na kuwapa mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato.

Waziri Kairuki amesema hivi sasa wapo katika mpango wa kujiendesha kibiashara kwa kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo maduka ya kuuza simu na ukopeshaji simu.

Akizungumzia mkongo wa taifa Waziri Kairuki amesema serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kusaini makubaliano na DRC kwa lengo la kuanza rasmi utoaji wa huduma za mkongo wa Taifa.

Amesema gharama ya kupeleka huduma hiyo katika jiji la Kinshasa inakadiriwa kufikia Sh bilioni 70, huku serikali ikiwa tayari imetenga Sh bilioni 30 katika mwaka huu wa fedha.”Kinshasa pekee ina wakazi zaidi ya milioni 10, hivyo ni soko kubwa na fursa muhimu ya kuongeza mapato ya taifa,” amesema .