March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Michezo inathibitisha umoja na maendeleo ya Taifa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 31, 2026 ameshiriki kwenye Azania Bank Bunge Bonanza 2026 linalofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Mkuu katika Bonanza la Bunge lililofanyika jijini Dodoma kwa ufadhili wa Benki ya Azania, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukivi, amesema michezo imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama nguzo ya mshikamano, umoja na maendeleo ya Taifa.

Amesema kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kuondoa mipasuko ya kijamii, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuongeza tija katika taasisi za umma na binafsi, akisisitiza kuwa mchango wake unaenda mbali zaidi ya burudani au mazoezi ya mwili.

Pia amewema kuwa pamoja na kujenga afya ya mwili ni njia madhubuti ya kupunguza msongo wa mawazo, kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, pamoja na kuimarisha afya ya akili kwa watumishi na jamii kwa ujumla.

“Msingi wa Bonanza la Bunge ni kuhimiza mshikamano na ushiriki wa jamii. Ushirikishwaji wa wabunge, watumishi wa Bunge, taasisi za Serikali pamoja na mashabiki wa Simba na Yanga ni mfano wa kuigwa katika kujenga umoja,” amesema.

Aidha, amezitaka taasisi za Serikali kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kudumisha michezo, kutenga muda rasmi wa michezo kazini na kuhamasisha ushiriki wa watumishi wote kama sehemu ya uwekezaji wa rasilimali watu.

Amesema kupitia michezo, watu wa kada, mitazamo na itikadi tofauti hukutana katika jukwaa moja, hali inayochangia kuimarika kwa mshikamano, utu na ushirikiano kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sirro, amesema michezo ni sehemu ya uongozi bora kwani hujenga afya ya viongozi na kuimarisha mahusiano kazini

Bonanza hilo limewahusisha Waheshimiwa Wabunge, Watumishi wa Ofisi ya Bunge, Taasisi mbalimbali pamoja na wananchi.

Kaulimbiu ya bonanza hilo ni “UMOJA WETU NI NGUVU YETU.”