March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taifa Stars yapokewa kwa heshima kubwa Dar

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, jana kiliwasili nchini kikitokea Morocco kwenye michuano ya AFCON 2025.

Stars iliwasili majira ya saa nne asubuhi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, baada ya kushiriki michuano hiyo.

Hata hivyo kikosi cha Stars kilipokelewa kwa heshima kubwa baada ya kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza.

Timu hiyo ilipokelewa na Mashabiki, Wadau wa michezo pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali waliokusanyika Uwanja wa Ndege kuilaki timu yao.

Akizungumza mara baada ya kukipokea kikosi hicho leo, waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya timu washindani wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), baada ya Timu ya Taifa, Taifa Stars, kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.

Kabudi amesema, wachezaji wameonesha kiwango cha juu cha ushindani, nidhamu na kujitoa kwa hali ya juu, hali iliyolipa taifa heshima kubwa barani Afrika.

“Taifa Stars wameonesha umahiri wa hali ya juu na kujitoa kwa hali yao yote. Kwa mafanikio haya, Tanzania sasa si mshiriki tu wa AFCON, bali ni mshindani wa kweli,” amesema Profesa Kabudi.

Amesema, mafanikio hayo ni ushindi mkubwa kwa taifa na yameweka msingi imara wa maandalizi ya AFCON ijayo ya 2027 itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.

Aidha, amesema Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo maalumu ya mapokezi ya timu hiyo na amepanga kukutana na kikosi cha Taifa Stars kesho kwa chakula cha mchana, kama ishara ya kutambua mchango wao kwa taifa.

Amewashukuru wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kuipokea timu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, ameipongeza timu hiyo kwa juhudi kubwa walizoonesha katika michezo waliyocheza licha ya changamoto walizokutana nazo katika mashindano hayo.

Mwinjuma amesema, lengo kuu la Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni kuhakikisha Taifa Stars inaendelea kukua na kupata uzoefu zaidi kimataifa.

Amesisitiza kuwa kushiriki mashindano makubwa kama AFCON ni sehemu ya mchakato wa kujenga Timu imara kwa siku zijazo.

“Lengo letu kubwa ni kuijenga Taifa Stars iwe timu imara kwa sasa na baadaye. Mashindano haya yametupa uzoefu mkubwa, na tunatambua bado tuna safari ndefu, lakini tupo kwenye mwelekeo sahihi.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa michezo kuhakikisha timu yetu inapata mazingira bora na mafanikio zaidi kwa taifa letu,” amesema Mwinjuma.