March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiruswa: Madini yachangia zaidi ya Asilimia 90 ya Sekta ya Ujenzi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema sekta ya ujenzi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki imejengwa kwa kiwango kikubwa na rasilimali madini, na kwamba Serikali imejipanga kuendelea kuboresha mazingira ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi.

Akizungumza katika Tuzo za Afrika Mashariki za Sekta ya Ujenzi, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Dkt. Kiruswa alisema bidhaa zinazotumiwa na wajenzi kwa zaidi ya asilimia 90 zinatokana na madini, ikiwemo mchanga, kokoto, mawe pamoja na bidhaa za viwandani kama tiles, nondo, mabati, malumalu na misumari.

Amesema Wizara ya Madini imekusudia kuhakikisha utajiri wa madini uliopo nchini unawanufaisha Watanzania moja kwa moja kupitia matumizi na biashara ya rasilimali hizo ndani na nje ya nchi.“Kila kitu wanachotumia wajenzi, zaidi ya asilimia 90 kinatokana na madini.

Sisi kama Wizara tumejipanga kuboresha sera zetu ili kuendelea kujenga mazingira rafiki kwa watumiaji wa rasilimali madini, kukuza uchumi na kuendeleza taifa letu,” amesema Kiruswa.Aidha, alisisitiza kuwa kabla ya mtu kupewa leseni ya uchimbaji, ni lazima awasilishe taarifa za uchambuzi wa athari za mazingira, iwe ni uchimbaji mdogo au mkubwa.

Kwa upande wake, Steven Mkomwa, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Sekta ya Ujenzi na Miundombinu Tanzania (CCIT), amesema huu ni msimu wa nne wa tuzo hizo zinazoshirikisha makampuni mbalimbali pamoja na watu zaidi ya 400 kutoka Afrika Mashariki.

Amebainisha kuwa tuzo hizo zimekuwa kichocheo muhimu katika kukuza ushindani na kuimarisha maendeleo ya sekta ya ujenzi.“Tuzo hizi zinachagiza sekta hii kwa kuwa washiriki wamekuwa wakichuana kupitia upigaji kura.

Tunaamini wale ambao hawakufanya vizuri safari hii watajipanga kufanya vizuri zaidi, na hatimaye kuchochea uchumi wetu,” amesema Mkomwa.

Naye Mwenyekiti wa CCIT, Pamela Shoo, amesema sekta ya ujenzi na miundombinu imekuwa ikionekana kama eneo la wakandarasi pekee, ilhali wapo wadau wengi wanaohusika, ikiwa ni pamoja na watengenezaji wa matofali na hata walio katika sekta ya madini. Alisema tuzo hizo zimetoa nafasi kwa wadau wote kutambulika na kuthaminiwa sawa.