March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu Rais wa pili Zanzibar apongeza Yas Zanzibar Marathon

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amepongeza maandalizi na mafanikio ya mbio za Yas Zanzibar International Marathon, ambazo zilifanyika visiwani Zanzibar kwa mafanikio makubwa.

Abdulla, ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha msimu wa tano wa mbio hizo jambo ambalo limeendelea kuimarisha nafasi ya Zanzibar kama kitovu cha utalii kupitia michezo na kuchochea afya na uchumi wa wananchi.

“Niwapongeze sana kwa maandalizi mazuri waandaaji wa mbio hizi pamoja na taasisi zote zilizoshiriki kuhakikisha Yas Zanzibar International Marathon inafana.

“Kama mnavyofahamu, mbio hizi zimekuwa ni jukwaa muhimu katika kuimarisha afya, kuchochea Utalii, kukuza uchumi na kuitangaza Zanzibar kimataifa. Hivyo tuna kila sababu ya kujivunia mbio hizi na kuhakikisha zinakuwa chachu ya maendeleo ya Zanzibar,” amesema Abdulla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma amesema Yas Zanzibar International Marathon imesaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ari ya michezo na kukuza Utalii wa Zanzibar.

Amebainisha kuwa, mbio hizo ni jukwaa muhimu kwa wanariadha kutoka maeneo mbalimbali kuonyesha vipaji vyao na kutambulika kimataifa kwani mbio hizo zimesajiliwa na Shirikisho la riadha duniani (World Athletic).

Kwa mwaka huu, mbio hizo zimevutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali ukiachana na Zanzibar, Tanzania Bara na nchi nyingine ni pamoja na Kenya, Sudan Kusini, Uganda, Uingereza, Ufaransa, Afrika Kusini, Marekani, Italia, India, China, Japan, n.k huku maelfu ya wananchi wakijitokeza kushiriki katika mbio hizo.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha amesema mbio hizo zenye kauli mbiu ya ‘Kila Hatua ni Spesho’ kwa mwaka huu wa 2025, zimeendelea kuwa zaidi ya ushindani wa riadha.

“Msimu huu wa tano umeonyesha thamani ya kauli mbiu yetu ya Kila Hatua ni Spesho. Kila mshiriki amekuwa sehemu ya hadithi ya mafanikio ya Zanzibar, kutoka kwa mkazi wa Pemba aliyekimbia kwa mara ya kwanza, vijana kwa wazee ambao wamethibitisha kuwa umri si kikwazo” amesema Pesha.

Ameongeza kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee tangu kubadilika kwa chapa, Yas na Mixx zimeona mafanikio makubwa kupitia Ushirikiao na Serikali ya Zanzibar.

“Tumepanua huduma za 4G na 5G kote Zanzibar, tumejenga minara 42 mipya kupitia UCSAF kuunganisha jamii za pembezoni, na zaidi ya Wazanzibari 25,000 sasa wanajipatia kipato kupitia mfumo wa biashara wa Yas na Mixx.

“Tumefanikisha malipo ya zaidi ya wakulima wa karafuu 100,000 kwa njia ya kidijitali, sambamba na kuchangia bima ya afya kwa maelfu ya wanufaika.

“Pia, tumeboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia suluhu za TEHAMA, na tumewezesha shule zaidi ya 40 kupata intaneti ya bure. Mafanikio haya yanaonyesha wazi dhamira yetu ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Zanzibar”.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Yas Zanzibar International Marathon, Hassan Bondi amemshukuru Rais kwa kushirika katika mbio hizo na vilevile aliwapongeza washindi na kuwashukuru washirika wa mbio hizi wakiwemo Yas na Mixx, Zanfastferries, GSM Beverages na Mnana Online TV ambao ni washirika wakuu wa mbio hizo.

“Tunawashukuru sana washirika wetu na wakimbiaji wote kwa kuungana nasi katika juhudi za kuchochea Utalii, Michezo, Afya na Biashara hapa Zanzibar alisema Bondi.

Washindi wa mbio wa Yas Zanzibar International Marathon kwa mwaka 2025Kilometa 21 (wanawake): Catherine Syokau raia wa Kenya Kilometa 21.

(wanaume): Maohhando Ako raia wa TanzaniaKilometa 10 (wanawake): Sisila Ginoka, raia wa TanzaniaKilometa 10 (wanaume): Mathias Sylvester, raia wa Tanzania.

Uwepo wa washiriki wa kimataifa na wa ndani katika mbio hizi umechochea ongezeko kubwa la wageni katika hoteli, migahawa, usafiri na biashara mbalimbali zilizopo Zanzibar.