March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaji wa Tanzania na Uingereza wakutana

MAJAJI wa Tanzania na Majaji wa Uingereza wamekutana jijini Dodoma  ili kuzungumzia masuala mbalimbali ya kijinai ambayo yana uzito katika nchi zao lakini pia kujenga misingi ya ushirikiano baina ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama  ya Uingereza.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Jaji  Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma wakati akifungua mkutano huo .

Profesa Ibrahim amesema,katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa katika mada zitakazotolewa katika mkutano huo zinazohusu mifumo ya mahakama ya nchi hizo mbili.

Alitaja mada zitaazotolewa kuwa ni pamoja na  kupata historia ya maboresho  kesi jinai katika kuangalia walipotoka, walipo ,wanakoelekea na changamoto zinazowakabili katika eneo hilo  ambapo mahakama ya Tanzania itatoa uzoefu wake katika eneno hilo na baadaye mahakama ya Uingereza itatoa uzoefu katika  eneo la kesi za jinai ambapo kwa Tanzania  kuna ucheleweshaji wa kesi hizo .

“Hapa tutaona zile hatua za awali kabla ya kesi kwenda kusikilizwa Mahakama Kuu ,sisi  tumekumbana sana na ucheleweshaji huo…, tukaona pengine wenzetu wa Uingereza watatusadia wao wanafanyaje katika kuhakikisha kwamba mfumo wao unaenda haraka .”amesema na kuongeza kuwa

“Pia wenzetu wa Uingereza watatuonyesha namna ya uendeshaji kwa hali ya kupunguza ucheleweshaji …,hili eneo ni muhimu sana hapa kwetu Tanzania tuweze kujifunza wenzetu wanafanya nini .”

Vile vile Profesa Ibrahim amesema,pia Majaji wa Uingereza watazungumzia suala la dhamana ambapo watatoa mfano Uingereza wanafanyaje katika suala la dhamana huku majaji wa Tanzania wao wataangalia dhamana kwa jicho na sheria za Tanzania zinasemaje .

Pia amesema Majaji wan chi hizo mbili watazungumzia  suala la fedha iliyopatikana katika uhalifu ambapo kila upande utatoa uzoefu wake.

“Suala hili nalo litazungumzwa na Jaji wa Mahakama  kuu ya Tanzania.., pia tutapata upande wa Uingereza wao wanafanyaje kuhusu masuala hayo,

“Lakini pia mkutano huu utazungumzia suala la uhalifu wa Kimataifa …, hili ni eneo muhimu katika ushirikiano kwani kuna aina za uhalifu ambazo ni za kimataifa ambapo bila ushirikiano nchi moja peke yake haiwezi kufanikiwa…, mfano kuna usafirishaji wa watu wazima ,kesi za usafirishaji watoto .”amesema Profesa Ibrahim

Aidha Jaji Mkuu huyo amesema,suala lingine muhimu wanaloenda kuliangazia kwenye mkutano huo ni  suala la kuwalinda mashahidi ambapo majaji wa nchi zote mbili watatoa uzoefu wao katika eneno hilo.

Amezungumzia suala la adhabu ambapo amesema litaangaliwa na kujadiliwa ili adhabu inapotolewa isitofautiane sana katika kosa linalofanana.

“Kwa bahati nzuri Serikali ya Uingereza ilitusaidia tukatengeneza muongozo wa kutoa adhabu ,huo ni mfano wa ushirikiano baina ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uingereza na Serikali ya Uingereza, wamewezesha sisi kutengeneza muongozo wa adhabu ambao unatakiwa kuwasaidia mahakakimu na majaji wanapotoa adhabu wasitoe adhabu zinazotofautiana sana katika kosa linalofanana .”

Mkutano umeandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Mahakama ya Uingereza na kuratibiwa na Taasisi ya Majaji Wastaafu ya nchini Uingereza iitwayo Slynn Foundation wakishirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kupitia Ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya kuzijengea uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT).