Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imekuwa ya kimkakati na imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 28,2026 amesema ziara hiyo imeimarisha uhusiano wa kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Urusi, huku nchi hizo zikisaini mikataba mbalimbali katika sekta za kimkakati za uchumi ambayo itanufaisha pande zote.
Amesema mafanikio ya ziara hiyo yanakuja wakati Tanzania ikijiandaa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya nchi kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja, kuongeza wastani wa pato la mtu kutoka dola 1,346.7 za sasa hadi dola 7,000 kwa mwaka, pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi katika sekta za afya, elimu, maji, nishati na hifadhi ya jamii.

Msigwa amesema kupitia Dira hiyo, Tanzania inalenga kuongeza wastani wa umri wa kuishi hadi miaka 75, kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa kwa asilimia 100, kutoa huduma za maji safi na salama kwa wananchi wote, pamoja na kufikia kinga ya jamii kwa asilimia 100.
Aidha, amesema sekta ya nishati ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi kupitia ushirikiano mpya na Urusi, ambapo nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika uchimbaji na uchakataji wa madini ya urani yanayopatikana kwa wingi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuchangia kufikia lengo la Tanzania la kuzalisha megawati 70,000 za umeme ifikapo mwaka 2050 kutoka megawati 4,032 za sasa, huku matumizi ya umeme kwa mtu yakiongezeka kutoka kilowati 256 hadi kilowati 3,000.

Msigwa amesema Urusi ni miongoni mwa mataifa kumi yenye uchumi mkubwa duniani, ikiwa na uchumi unaokadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni 2.65 na wastani wa pato la mtu wa dola 18,525 kwa mwaka, hivyo ushirikiano huo utafungua fursa mpya za uwekezaji, biashara, teknolojia na maendeleo ya viwanda kwa Tanzania.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutumia diplomasia ya uchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuvutia uwekezaji, kuongeza biashara na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

More Stories
Yas Business,FTCC wawajengea uwezo Wajasiriamali
Msigwa:Kiwango uchumi wa kujitegemea kimeongezeka nchini
Ndejembi:Miradi mikubwa kuipa nguvu Gridi ya Taifa