Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kujenga uchumi wa kujitegemea, ambapo kiwango cha kujitegemea kwa uchumi kimeongezeka kutoka chini ya asilimia 50 miaka michache iliyopita hadi kufikia asilimia 74.2 kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 28,2026 ambapo amesema mafanikio hayo ni uthibitisho wa utekelezaji mzuri wa sera na mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha uchumi wa Taifa na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia maendeleo yake.

Amesema hali ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania inaendelea kuwa imara, ambapo mwaka 2025 uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 5.9 na matarajio ni kufikia ukuaji wa asilimia 6.3 mwaka 2026 kutokana na kuendelea kwa uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, amesema mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kufikia wastani wa asilimia 3.4 hadi Machi 2026, kiwango ambacho kiko ndani ya lengo la Serikali la asilimia tano, hali inayochangia utulivu wa bei za bidhaa na huduma.
Msigwa pia amesema akiba ya fedha za kigeni imefikia dola za Marekani bilioni 5.72, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 4.4, huku thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani ikiendelea kuimarika kwa wastani wa asilimia 2.7.
Amesisitiza kuwa viashiria hivyo vinaonyesha uimara wa uchumi wa Taifa na matokeo ya juhudi za Serikali katika kuimarisha uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kusimamia sera za uchumi zinazolenga ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya nchi.


More Stories
Yas Business,FTCC wawajengea uwezo Wajasiriamali
Ziara ya Rais Samia Urusi yaleta fursa mpya
Ndejembi:Miradi mikubwa kuipa nguvu Gridi ya Taifa