November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Rais Samia nchini India yaleta neema ya uwekeaji

Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online,Dar

ZIARA za Rais Samia Suluhu Hassan, nje ya nchi zimeendelea kuzaa matunda baada ya Kampuni ya ES kutoka India kuja nchini kwa ajili ya uwekezaji kwenye ya sekta ya afya.

Kampuni hiyo inatarajia kuwekeza dola milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha dawa za binadamu, ujenzi wa chuo na kuifanyia maboresho ya hospitali ya Tanzanite ya Jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uhamasishaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),John Mnali, amesema wawekezaji hao pia wanatarajia kuja na madaktari bobezi 10.

Amesema wawekezaji kutoka kampuni ya ES wameingia nchini jana, kwa lengo likiwa ni kuanza kufanya upembuzi yakinifu na mradi huo unatarajiwa kuanza Aprili, mwaka huu.

“Tumekutana na wawekezaji kutoka nchini India ambao ni kampuni ya ES ambayo itashirikiana na Tanzanite hospitali iliyopo Mwanza. Tutahakikisha wawekezaji hao wanapata vibali na leseni zote muhimu ambazo wanazihitaji ili uwekezaji huo uweze kukamilia,”amesema

Aidha, Mnali amesema uwekezaji huo ni matokeo ya ziara zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nje ya nchi. Mnali alihamasisha wawekezaji wa ndani kuanzasisha miradi mbalimbali na kupanua shughuli zao, kwa sababu TIC itaendelea kutoa ushirikiano.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali ya Tanzanite, Jared Awando, amesema mkataba wa uwekezaji huo ni wa miaka mitatu na kwa kuanzia utaboresha hospitali ya Tanzanite na ununuzi wa vifaa.

Pia Awando amesema,huduma zitakazotolewa hospitalini hapo baada ya uwekezaji huo zitasaidia kupunguza safari za Watanzania kwenda nje ya nchi kupatiwa matibabu.

Awando aliongeza kuwa, wawekezaji hao na madaktari bingwa wanatarajia kuanza kazi mwezi wa nne na baadhi ya huduma bobezi zitakazotolewa ni za meno na macho.

Aidha ametoa rai kwa wafanyabiashara nchini wanaotaka kuwekeza kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki ziara mbalimbali zinazofanywa na Rais Dk. Samia na TIC nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ES, Pina Vyas, alishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kampuni hiyo itahakikisha inaleta uwekezaji wenye tija.

Pia Pina amesema ES itahakikisha inafanya kazi kwa kushirikina na hospitali ya Tanzanite na Serikali kwa ujumla.

“Nafurahi kupata nafasi ya kuwekeza Tanzania tumejipanga kufanya kazi vizuri na kwa kushirikiana tutawekeza katika sekta ya afya hospitali ya Tanzanite na kujenga kiwanda cha dawa za binadamu.”