Na Salma Lusang, Zanzibar
MKURUGENZI Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ali Said amesema ZHC imeanza harakati za ujenzi wa nyumba 72 za makazi katika eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja ili kuwaletea wananchi wa Zanzibar makazi bora.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na muandishi wa habari hizi, Mkurugenzi huyo alisema harakati za ujenzi wa nyumba hizo zimeanza Mwezi Machi mwaka huu ambapo shirika hilo limefunga mkataba wa ujenzi na Mkandarasi Simba Developers Ltd. Hivyo Mkandarasi huyo ameanza kazi rasmi.
Mkurugenzi Mwanaisha alisema ujenzi huo utagharimu shilingi za Tanzania bilioni tisa nukta nane (9.8) hadi kumalizika kwake kati ya fedha hizo shilingi bilioni tatu (3) zitatoka katika mfuko wa ZHC na fedha zingine zimetoka katika mfuko wa Serikali kuu kwa maana ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dkt, Hussein Ali Mwinyi.
Alifahamisha kwamba ZHC imekubaliana na Mkandarasi huyo katika kipindi cha muda wa miezi 15 kuanzia Machi 2023 nyumba hizo ziwe zimekamilika ili shirika liweze kuziuza nyumba hizo kwa wananchi mbali mbali ambao watahitaji kununua.
“ Lengo letu ni kuziuza nyumba hizo kwa mwenye kuhitaji, pesa za ujenzi Bilioni tatu tumetoa ZHC na fedha zingine tumepewa na Serikali kuu, nyumba zote zitakua 72 mtu pesa zake tu”. Alisema Mwanaisha.
Aidha Mkurugenzi Mwanaisha alisema bei ya kuziuza nyumba hizo zitatofautiana kwa sababu kutakuwa na nyumba za vyumba vitatu na zingine vyumba viwili ila kiwango cha bei itapangwa na Serikali baada ya ujenzi kukamilika.
Naye Meneja Mkuu wa kampuni ya Simba Developers Ltd Nurdin Hussein ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuiamini kampuni yake na kuipa dhamana ya kujenga nyumba hizo. Hivyo ameahidi kwamba kampuni yake itafanya kazi kwa ufanisi na kwa wakati muwafaka kama walivyokubalina na ZHC.
Kwa Upande wa wananchi wa Zanzibar, akizungumza Bi Asha Ali Kombo (51) Mkaazi wa Fuoni Uwandani ameishukuru Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wa kujenga nyumba mpya kwani ni wazi kwamba Nyumba za Maendeleo Zanzibar ni chache na kongwe hivyo hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kwa Shirika la Nyumba Zanzibar.
Naye Omar Ali Issa (48) Mkaazi wa Rahaleo aliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka mpango wa kuwauzia watu kwa kulipa fedha kidogo kidogo kwa wenye kipato cha chini.
Alieleza kwamba kutokana na kipato tofauti baadhi ya watu hawataweza kutoa kiwango kikubwa cha fedha kwa pamoja ila kwa kulipa nusu nusu wataweza.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini