May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zeche aikimbia CHADEMA ahamia CCM

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online. Dar

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, Aprili 17, 2024, ametoa pongezi kwa Zeche Chengula, kufuatia hatua alio chukua ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA).

Zeche ambaye ametajwa kuwa kiongozi wa Machinga mkoani Iringa na aliyekuwa mwanachama wa CHADEMA.

Dkt.Nchimbi ametoa pongezi hizo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Nzovwe jijini Mbeya, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya CCM katika mikoa sita.

” Nampongeza Zeche kwa maamuzi yake aliyofanya ya kuhamia katika chama cha wapendwa haki na maendeleo CCM…kule alipokuwa siyo dhambi lakini huku alipokuja ni kuzuri zaidi, hivyo tunakila sababu ya kumpongeza na tunawakaribisha wote wanaopenda maendeleo ya nchi yetu CCM,”amesema Nchimbi.

Sanjari na hayo, Nchimbi ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Mbeya kuwa na ushirikiano wao pamoja na kwa viongozi ili kuweza kuleta maendeleo katika Jiji hilo na Tanzania kwa ujumla.

Amesema, ni vyema kila mmoja akatambua na kufanya wajibu wake kwa kushirikiana katika kuleta maendeleo, huku akiwataka vijana kuachana na dhana ya kuwa tegemezi na badala yake wajitume kwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali zitakazo waingizia kipato kihalali.

Hivyo amewahimiza kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ambayo Rais Dkt. Samia ameirudisha ambayo inaanza kutolewa tena katika halmashauri zote nchini.

Hata hivyo amewataka viongozi kuwa waadilifu katika matumizi ya mali za umma kwa manufaa ya Taifa.

“Wengi wamekuwa wakioata madaraka, wamekuwa wakitumia vibaya mali za umma jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya nchi hivyo ni vyema kuwa waaminifu ili tuweze kuwatumikia vizuri wananchi wetu na kulinda mali”, amesema Nchimbi.

Akieleza sababu za yeye kukihama chama chake cha awali Zeche Chengula, amedai kuwa mbali na kuwa mjasiriamali, pia amekuwa mwanaharakati kwa kipindi cha muda mrefu huku akidai kutumiwa vibaya na moja ya chama pinzani bila manufaa yoyote ya nchi kwa ujumla.

Amedai moja ya sababu iliomfanya kuhamia CCM ni baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa chama hicho na kudai kutoa ushirikiano ikiwa pamoja na elimu kwa vijana wengine kuachana na siasa chafu za kutumiwa na vyama pinzani.

“Nimechoka kutumiwa na chama ambacho nilikuwa mwanachama wake hapo mwanzo, kwa sababu sisi kama vijana na machinga tumekuwa wakitutumia sana kwenye kuandamana kwa ajili ya maslahi yao binafsi alafu hakuna maendeleo yoyote ambayo wamekuwa wakituletea,”amesema Chengula.

Aidha ametoa wito kwa machinga na vijana wengine, kukataa kutumika katika siasa chafu bila ya kujua wanawanufaisha viongozi wa chama husika na si wananchi kwa ujumla kwa kuwaletea maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, amewataka wananchi wa Mbeya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya ikiwa pamoja kuleta miradi ya maendeleo katika Jiji hilo na mingine ikiwa imekamilika pamoja na kuwa kwenye hatua za mwisho za ukamilikaji.

Pia amewatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa Jiji hilo lipo salama na wananchi wameendelea kujikita katika shughuli zao za kila siku kwa amani na utulivu ikiwa pamoja na shughuli za kilimo.