Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi amesema watu zaidi ya milioni moja hapa nchini wamechanja chanjo ya Johnson Johnson (JJ) kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.
Profesa Makubi amebainisha hayo leo wakati akizungumza kwenye mkutano ulioikutanisha Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto na Wadau wa mashirika yasiyo ya Kiserikali ili kujadiliana katika kuwafikia wananchi kuwapa elimu kuhusu chanjo UVIKO 19 aina ya Sinopharm.
Amesema,chanjo ya JJ imesha hivyo chanjo inayotolewa sasa ni aina ya Sinopharm ambayo dozi yake inachanjwa mara mbili.
“Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinia na Watoto leo imekutana na Wizara ya Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa lengo la kushirikishana kuhusu mapambano dhidi ya UVIKO 19 lengo kubwa likiwa ni kuongeza idadi ya watu kuchanja.”amesema Profesa Makubi na kuongeza kuwa
“JJ imeisha ,sasa tunachanja Sinopharm,kazi iliyopo ni kuhamasihsa wananchi warudi mara mbili kupata chanjo ili kukamilisha dozi ya Sinopharm.”amesema na kuongeza kuwa
“Hii ni kazi kubwa ,tumeona tuwashirikishe wadau wa sekta binafsi ili tushirikiane katika kuhamasisha kwa kutoa elimu ili wananchi wengi wajitokeze kwa wingi na waruidie kukamilisha dozi.”
Aidha amesema,kwa wananchi ambao tayari walishachanja JJ hawatakiwi kuchanja tena Sinopharm huku akisema hii ni kwa ajili ya wale ambao bado hawajachanja kabisa huku akisema chanjo ya awali walikuwa wakiwafikia watu 50,000 kwa siku ambapo lengo la sasa ni kuwafikia wananchi 100,000 kwa siku kuwapatia chanjo hiyo.
“Kwa muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Serikali,ukishachanja JJ hutakiwi kuchanja Sinopharm maana tayari umeshapata kinga na tiba zake ni sawa sawa.”amesema
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya Dkt.Grace Magembe amesema,katika awamu ya kwanza walitumia mkakati harakishi waliokuwa wameuandaa kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kwenda kuchanja na ulionyesha mafanikio.
Amesema,kutokana na mafanikio ya mkakati huo,katika awamu ya pili ya uchanjaji watatumia mkakati huo ili katika kuhamasisha wananchi kwenda kuchanja na kufikia malengo yaliyowekwa.
Akizungumza kwa niaba ya wadau kutoka Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nacongo)Dkt. Lilian Badi amesema,wao wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kampeni ya kuhamasisha wananchi kwenda kupata chanjo ili kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.
Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali iwawezeshe ili waweze kuifanya kazi hiyo ya kufikisha elimu kwa wananchi na kuikomboa nchi dhidi ya UVIKO 19.
“Sisi tunafanya kazi jamii na katika kampeni hii ya kuelimisha wananchi kwenda kupata chanjo ,tupo tayari kufanya kazi hii ila tunaiomba Serikali itupe ‘resouces’kwani uwezo wa kufikisha elimu kwa jamii tunao.”amesema Dkt.Badi
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi