May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya kilomita 100, za barabara zimefunguliwa Ilemela

Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Barabara takribani kilomita 126 zinazounganisha kata kwa kata,wilaya kwa wilaya jimboni Ilemela zimefunguliwa kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Ilemela.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa barabara kutoka ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,Mpunzi Mbegeje wakati wa zoezi la ufunguaji na uunganishaji wa mtandao wa barabara hizo ambazo zinatokea Buswelu Mbogamboga kupitia Nyamadoke kuelekea Nyamh’ongolo, ameeleza kuwa Mbunge anatambua changamoto za usafiri zinazokabili wananchi wake hasa kipindi cha mvua.

Mratibu wa barabara kutoka ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,Mpunzi Mbegeje akiwa katika moja ya barabara wakati wa zoezi la ufunguaji na uunganishaji wa mtandao wa barabara zinatokea Buswelu Mbogamboga kupitia Nyamadoke kuelekea Nyamh’ongolo.

Ambapo ameeleza kuwa ufunguaji na uunganishaji wa mtandao huo wa barabara utasaidia wananchi wa jimbo hilo kuwa na uhakika wa usafiri wakati wote hivyo kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii za kila siku.

Ameeleza kuwa,Mbunge huyo amekuwa akishiriki katika kufungua barabara hizo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa kile alichowaahidi wananchi wakati anawaomba kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Sanjari na hayo ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza bajeti ya Mfuko wa Jimbo na ya TARURA kwa Wilaya ya Ilemela ili kukidhi mahitaji ya wananchi na uhitaji uliopo.

“Wilaya hii imekuwa ikikua kwa kasi siku hadi siku jambo linalomlazimu wakati mwengine Mbunge wa jimbo hilo kutoa fedha zake binafsi au kushirikiana na wadau wa maendeleo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara,”ameeleza Mbegeje.

Moja ya barabara zilizofunguliwa wilayani Ilemela.

Kwa upande wake Msimamizi wa ufunguzi wa mtandao huo wa barabara kutoka TARURA Wilaya ya Ilemela Mhandisi Said Tano Irema,ameeleza wameisha pokea barabara 47 zilizofunguliwa na Mbunge huyo kwa ajili ya kuzihudumia kama mamlaka ya usimamizi wa barabara ndani ya wilaya hiyo.

Mmoja wa wananchi kutoka Kata ya Kahama Rubanila Matoforo ambaye ni dereva bodaboda ameishukuru serikali kwa ukarabati wa barabara ya kutoka Kahama senta kuelekea Isela itakayosaidia kuwainua kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa bidhaa na huduma kutoka kwenye makazi yao kuelekea soko kuu la Buswelu.

Huku Amina Songe amempongeza Mbunge wa Ilemela kutatua changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili hasa kwa wajawazito wakati wa kujifingua wakitokea eneo la Isela kuelekea zahanati ya Kahama.