Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, imewatambua wafanyakazi waliofanya vizuri katika kutoa huduma kwa wateja kwa mwaka 2026.
Hata hivyo imesisitiza umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha uwezo wao wa kutatua changamoto za wateja.
Hafla hiyo imefanyika mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam, ikiwa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Lengo likiwa kuthamini mchango wa watoa huduma katika kuwasaidia wateja na kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Yas, Mwangaza Matotola, amesema ukuaji wa sekta ya mawasiliano na mabadiliko ya teknolojia yanahitaji wahudumu kuendelea kuongezewa ujuzi ili kuwahudumia vizuri wateja wa Yas na Mixx.
Matotola amesema, ingawa huduma kwa wateja imepiga hatua ikilinganishwa na miaka iliyopita, bado kuna haja ya kuimarisha mafunzo ili wahudumu waweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka.
Amesema, maendeleo ya teknolojia yameleta manufaa kwa watumiaji, lakini pia yameibua changamoto zinazohitaji wahudumu kuwa na uelewa wa kutosha wa huduma za Yas na Mixx pamoja na mabadiliko yake.
Kwa upande wake, Anna Kulinganila, mmoja wa wafanyakazi waliotambuliwa kwa kufanya vizuri katika huduma kwa wateja, amesema kumekuwa na mabadiliko katika namna wateja wanavyowasiliana na wahudumu wanapohitaji msaada.
Amesema, simu zenye matusi na lugha zisizo na staha zimepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita, ingawa bado wanakutana na baadhi ya wateja wanaotumia lugha isiyofaa.

More Stories
Homera ashiriki mkutano wa 17 jukwaa la kimataifa Nishati
EWURA yaeleza sababu kutangaza bei za mafuta
Kampeni ‘Ongea na Kamanda’ yazinduliwa Mwanza