August 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas Fiber yazindua huduma Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKAZI i na wafanyabiashara wa Dodoma wamepata fursa nyingine ya kutumia intaneti yenye kasi na uhakika baada ya Kampuni ya Yas Fiber kuzindua rasmi huduma zake jijini humo.

Huduma hiyo, ambayo kwa kuanzia inapatikana maeneo ya Ilazo, Ipagala, Swaswa na Mjini Kati na Barabara za namba, inalenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya intaneti katika jiji hilo linaloendelea kukua kupitia makazi, biashara na taasisi.

Kupatikana kwa huduma ya Yas Fiber kunatarajiwa kurahisisha shughuli mbalimbali zinazotegemea intaneti, ikiwemo biashara, elimu kwa njia ya mtandao, kufanya kazi ukiwa nyumbani na matumizi ya huduma mbalimbali za kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ukuaji wa Dodoma unahitaji kwenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya mawasiliano.

“Dodoma inakua kwa kasi na ukuaji huu unahitaji kwenda sambamba na miundombinu ya uhakika, ikiwemo huduma za mawasiliano ya kidijitali.

*Uwekezaji kama huu wa Yas Fiber utawasaidia kwa kiasi kikubwa wakazi wa Dodoma, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kutumia fursa zinazopatikana katika uchumi wa kidijitali,” amesema Shekimweri.

Amesema, vijana na wajasiriamali ni miongoni mwa makundi yanayoweza kunufaika zaidi na huduma hiyo kupitia upatikanaji wa elimu, taarifa, masoko na huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Fiber, Maxime Woimant, amesema kampuni hiyo imeamua kupeleka huduma Dodoma kutokana na ukuaji wa jiji hilo na kuongezeka kwa mahitaji ya intaneti yenye kasi na uhakika.

“Hatujaleta tu intaneti yenye kasi Dodoma. Tumeleta huduma inayoweza kumsaidia mwananchi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, mwanafunzi kujifunza na mfanyabiashara kukuza biashara yake na kuwafikia wateja wengi zaidi,” amesema Woimant.

Amesema, huduma hiyo inaweza kuwasaidia wafanyabiashara kutumia mifumo ya kidijitali, kutangaza bidhaa na huduma zao na kuwafikia wateja kupitia mtandao.

Katika hatua nyingine, Yas Fiber imetangaza kuwa wateja wake sasa watapata data ya simu na dakika za kupiga mitandao yote kupitia namba zao za Yas bila gharama ya ziada, kama sehemu ya vifurushi vyao vya Fiber vya kila mwezi.

Kulingana na kifurushi atakachochagua mteja, atapata hadi GB 30 za data pamoja na hadi 500 za kupiga mitandao yote, kwa mwezi huku bei ya huduma ya Fiber ikibaki vilevile.