Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka watafiti katika sekta ya usafiri na usafirishaji kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto halisi, ikiwemo kupunguza gharama za lojistiki na kuongeza ufanisi wa miundombinu ya usafiri nchini.
Profesa Mbarawa ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Usafiri, Lojistiki na Usimamizi, lililoandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Amesema Serikali inasisitiza umuhimu wa tafiti zinazoweza kubadilisha maarifa kuwa vitendo na kutoa matokeo yanayopimika, badala ya tafiti zinazoishia kwenye taarifa na kuhifadhiwa kwenye makabrasha.
“Usafiri si suala la kuhamisha watu na mizigo kutoka eneo moja kwenda jingine pekee, bali ni kichocheo cha biashara, uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi kwa ujumla,”Amesema.
Profesa Mbarawa amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali za usafiri, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uboreshaji wa bandari, kuimarisha Air Tanzania, mfumo wa mabasi yaendayo haraka (BRT), barabara, usafiri wa majini na uchumi wa buluu.

Amesema lengo si kujenga miundombinu pekee, bali kuunda mfumo mmoja wa usafiri uliounganishwa unaoshirikisha reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini.
“Mfumo huu unalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika usafiri na usafirishaji kwa kuhudumia masoko ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini,”Amesema.
Ameongeza kuwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Tanzania inahitaji mfumo wa usafiri utakaosaidia kujenga uchumi wenye ushindani, kukuza viwanda na biashara pamoja na kuimarisha uhusiano na masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, amesema miundombinu inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi, kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza muda wa mizigo kufika sokoni na kuboresha usalama pamoja na huduma kwa watumiaji.
“Thamani halisi ya miundombinu ni fursa za kiuchumi zinazozalishwa. Naweza kujenga miundombinu mingi lakini bila kuzalisha fursa za uchumi haina maana,” amesema.
Aidha, amewataka watafiti kutumia kongamano hilo kutoa mapendekezo yanayotekelezeka yatakayosaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha ufanisi wa bandari na reli, kuongeza usalama wa usafiri, kutumia teknolojia mpya na kujenga miundombinu inayoweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mabadiliko ya teknolojia za kidijitali, akili mnemba, uendeshaji wa kiotomatiki pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kubadilisha namna mifumo ya usafiri inavyopangwa na kuendeshwa.
Profesa Mbarawa amewahimiza washiriki kuhakikisha mafanikio ya kongamano hilo hayapimwi kwa idadi ya washiriki, muda wa mkutano au idadi ya mada zitakazowasilishwa, bali kwa suluhisho zitakazopatikana, sera zitakazoboreshwa na changamoto za usafiri zitakazopatiwa ufumbuzi kupitia tafiti.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema kongamano hilo ni la nne na limeendelea kukua kwa kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema idadi ya washiriki wa kimataifa imeongezeka kutoka wawili katika kongamano la kwanza lililofanyika mwaka 2023 hadi kufikia 16 mwaka huu.
“Ongezeko hili ni ishara kuwa kongamano hili sasa limejenga hadhi ya kimataifa, huku baadhi ya wataalamu wakitoka Japan na Uingereza kushiriki moja kwa moja katika kongamano hilo,” amesema Dkt. Mgaya.
Aidha, amesema Tanzania inahitaji kuimarisha muunganiko wa reli, usafiri wa anga na majini ili kuwezesha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kutumia miundombinu ya reli kufikisha mizigo katika maeneo ya mipakani na kuiunganisha na nchi jirani kama Burundi na Rwanda.
Dkt. Mgaya amesema kongamano hilo linatoa fursa kwa wataalamu kuwasilisha tafiti na kujadili changamoto zinazolikabili sekta ya usafirishaji, hatua inayotarajiwa kusaidia Serikali na sekta binafsi kupata suluhisho na kufanya maamuzi yenye tija.
“Tunatambua uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya katika kujenga miundombinu ya usafirishaji. Hata hivyo, miundombinu hii katika uendeshaji inahitaji maamuzi na usimamizi mzuri,”Amesema.
Ameongeza kuwa matokeo ya majadiliano na tafiti zitakazowasilishwa katika kongamano hilo yanaweza kutumiwa na Serikali pamoja na sekta binafsi kuboresha huduma na kukabiliana na changamoto za sekta ya usafirishaji.
Aidha, amemshukuru Waziri wa Uchukuzi, Profesa Mbarawa, kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono NIT, akisema juhudi za Wizara zimechangia pia kupatikana kwa wadhamini na kufanikisha kongamano hilo.
Amesema ushirikiano wa Serikali umekuwa muhimu katika kuhakikisha kongamano hilo linaendelea kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023.

More Stories
Yas Fiber yazindua huduma Dodoma
Kampuni ya Algeria kuwekeza viwanda vya korosho Tanzania
Nombo: Tanzania yaandaa vijana kushindana kimataifa