January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yanga yaendeleza ubabe Ligi ya NBC yailaza Mbeya Kwanza nyumbani kwao

Na Yusuph Digossi 

Licha ya kocha wa Yanga Nesrdin Nabi kuonesha wasiwasi juu ya hali ya uwanja wa Sokoine , hiyo haikuwa sababu kwa kikosi cha Yanga Sc kucheza soka safi na kuondoka na alama tatu muhimu baada ya kuichapa timu ya Mbeya Kwanza kwa mabao 2-0 na kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya NBC 2021-2022

Mabao ya Yanga yalipachikwa  Saido Ntibanzokiza dakika ya 17 kwa adhabu ndogo ya mpira wa kutenga baada ya kiungo Feisal Salum kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la 18 na Fiston Mayele akawainua tena wana Jangwani waliokuwa wamefurika katika uwanja wa Sokoine mnamo dakika ya 25 baada ya kuunganisha pasi safi ya kiungo Mzanzibari Feisal Salum. 

Ushindi huo unaifanya Yanga kujikita kileleni wakiwa na pointi zao 19 na kubaki palepale nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.

Yanga walianza mchezo kwa kasi ya chini lakini hawakwenda  mapumziko mikono mitupu  baada ya kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa mbele  kwa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza.

kabla ya mabao hayo kupatikana, Yanga ilitengeneza nafasi kadhaa lakini walikosa  umakini kwa kushindwa kutumia vyema nafasi mbili kupitia kwa Deus Kaseke aliyeshindwa kumalizia pasi ya Feisal dakika 18 na Mayele aliyekosa dakika ya kwanza alipopokea pasi ya faulo ya Ntibazonkiza.

Mbeya Kwanza kipindi cha kwanza walikosa umakini na kushindwa kuzitumia nafasi ambazo walizipata.

 Kipindi cha pili Mbeya  waliweza kutulia na kucheza kwa kushambulia ila safu ya ulinzi ua Yanga ilikuwa imara na kumaliza mchezo huo bila ya kuruhusu bao.

Mchezo huo unakuwa ni  wa kwanza kwa Mbeya Kwanza kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine na mchezo wa pili kwao kupoteza katika ligi.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha mkuu wa Yanga alisema kuwa siri pekee ya kupata alama 3 ni wachezaji kufuata maelekezo aliyowapatia wakiwa mazoezini. 

” Ninawapongeza wachezaji kwa kiwango bora katika mechi ya leo na walifanya kila kitu tulichokipanga mazoezini, tumepata alama tatu muhimu ingawa haikuwa mechi rahisi” alisema kocha Nabi

Akijibu swali la maandalizi yao kuelekea mchezo wa Kariakoo Dadi Disemba 11 kocha Nabi alisema kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia mchezo huo muda ukifika atazungumza kuelekea mechi hiyo

Wachezaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza ( wa nyuma) na Feisal Salum (mbele) wakishangilia bao la kwanza lililogungwa na Ntibazonkiza mnamo dakika 17 katika mchezo wa Ligi kuu ya NBC dhidi ya Mbeya kwanza ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa 2-0 (Picha na mtandao wa Yanga )Â