May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WWF yaja na mradi wa kurejesha uoto wa asili ukanda wa Mashariki

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Uharibifu wa mazingira katika maeneo mengi Nchini umetajwa kuwa ndio chanzo kinachopelekea wanyama ikiwemo Tembo kuhama kwenye makazi yao na kuingia kwenye makazi ya wananchi kwajili ya kutafuta maji na vyakula.

Kufuatia hatua hiyo Halmashauri ya wilaya ya Korogwe ni moja kati ya sehemu zilizoathirika tembo kuvamia makazi ya watu na kuharibu mazao ya wananchi pamoja na kusababisha vifo vya watu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Halfan Magani wakati akizindua mradi wa uhifadhi mazingira wa kurejesha uoto wa asili wa misitu ya ukanda wa Usambara mashariki katika wilaya ya Korogwe na Mkinga unaofadhiliwa na shirika la WWF.

Mkurugenzi Magani amesema kuwa suala la uharibifu wa mazingira ni jambo la kidunia huku Tanzania ikiwa sehemu mojawapo ya tatizo hilo .

Aidha amesema uharibifu wa mazingira una madhara mengi kwa binadamu kwani mazingira yanapoharibika hususani katika maeneo ambayo walikuwa wanaishi wanyama kama tembo wanakosa vitu vya msingi kama vyakula na maji hali inayopelekea wanayama kutoka kwenye misitu na kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni moja kati ya sehemu ilizoathirika sana na tembo kwakuwa wanalazimika kutoka kwenye hifadhi ya Mkomazi na kuingia kwenye makazi ya wananchi kutafuta maji hivyo wanachokutana nacho njiani wanaharibu ikiwemo mazao ya wananchi wetu, “Alisisitiza Mkurugenzi Magani.

Aliongeza kuwa nitumie fursa hii kuwapongeza WWF kwa kuja na mradi wa kuhifadhi mazingira ambayo mojawapo ya faida ni kwenda kuhuisha misitu ambayo baadaye tutakuwa tunazuia janga la tembo kutoka kwenye misitu kuja kwenye makazi ya binadamu.

Sambamba na hayo aliwataka wakazi wa Korogwe katika baadhi ya vijiji vitakavyofikiwa na mradi huo wananchi kuupokea na kuunga mkono kwasababu mradi huo ni majawapo ya sehemu inayokwenda kutatua changamoto ya Tembo.

Lakini pia Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi watakaohusishwa katika mradi huo kutoa ushirikiano ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia za kusisitiza wanatunza vyanzo vya maji kwani misitu ni mojawapo ya vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Meneja wa uhifadhi ambaye pia ni mratibu wa Programu ya misitu kutoka shirika la WWF Tanzania Laurance Mbwambo amesema moja ya visababishi vya uharibifu wa mazingira katika maeneo mengi ni kutokana na ongezeko la watu katika eneo dogo ambalo haliwezi kuhimili mahitaji yao.

Mwambo amesema kuwa takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza misitu takribani hekta laki 469000 hivyo ipo haja ya kuchukua tahadhari ndio maana shirika hilo la WWF limekuja na miradi ya kurejesha uoto wa asili miradi ambayo inalenga kurejesha uoto wa asili na kuboresha maisha ya watu.

Alisema WWF inakuja na teknolojia na mbinu mbadala za kupunguza makali ya maisha ya watu na sio kwa kutegemea tu misitu lakini pia watu wawe na uwezo wa kuzalisha chakula katika maeneo madogo kwa kuja na teknolojia ya kuzalisha chakula kingi kwenye eneo dogo na waweze kuzalisha kwa tija.

“Ni muhimu kuangalia idadi ya watu wanaoishi mahali fulani na maendeleo ambayo yanatakiwa kufanyika ni kazi ya serikali na wadau wengine kuangalia ni kiasi gani cha watu wanaweza kukaa kwenye eneo moja kwasababu wakati mwingine watu wamejirundika tu eneo moja kwamaana labda hawajui fursa nyingine zinazopatikana katika maeneo mengine, “alisema Mbwambo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuta wilayani Mkinga Emmanuel Simba amelishukuru shirika hilo kwa kuwafikishia mradi huo wa uhifadhi ambao wanatarajia utaleta manufaa makubwa kwao kwani katika maeneo mengi wanayoishi wamezungukwa na msitu huku wakiahidi kuhamasisha wananchi kuacha kukata kuni ovyo na kuchoma mikaa.

Mradi huo wa kurejesha uoto wa asili unatekelezwa katika wilaya mbili za Mkoa wa Tanga ikiwemo wilaya ya korogwe na Mkinga na unatazamiwa kuwa mradi wa miaka minne kwa kushirikisha jamii kwenye vijiji 10 ambavyo vitafanyiwa kazi.