Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), imeanza kampeni ya kuwaelimisha wajasiriamali wadogo kuhusu umuhimu wa kuwa na vipimo sahihi kwenye biashara zao.
Mafunzo hayo ambayo yatakuwa endelevu ili kuwafikia wajasiriamali wengi wadogo nchini yalifanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za WMA jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia umuhimu wa vipimo sahihi kwenye mafunzo hayo, Kaimu Meneja Upimaji, Pastory Almachus alisema vipimo sahihi hutumiwa na taasisi mbalimbali kwaajili ya kupata takwimu sahihi.
Alitoa mfano kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hutumia kigezo cha vipimo katika ukusanyaji mbalimbali wakati inapotoza kodi kwa bidhaa mbalimbali.
Alisema kwenye miundombinu na usafirishaji vyombo vya usafiri hubeba bidhaa, mizigo na abiria kulingana na uwezo hivyo kuepusha ajali na uharibifu wa miundombinu kama barabara na reli nakupunguza matukio ya ajali.
Alisema hata wakulima hutumia vipimo vilivyo sahihi katika matumizi ya pembejeo wakati wa uzalishaji na wakati wa kuuza mazao yake ili apate thamani kulingana na gharama alizotumia.
Aidha, taarifa zinazotolewa na sekta mbalimbali kuhusu uzalishaji, biashara na uchumi hutegemea vipimo nazo husaidia kujua mchango wa kila sekta katika pato la taifa kwa usahihi.
Alisema bidhaa zinazotengenezwa viwandani hutegemea vipimo ambavyo hutumika kupimia malighafi na mahitaji mengine na kwamba bidhaa zikishatengenezwa bado hutegemea usahihi wa vipimo wakati wa kufungashwa katika ujazo, urefu au uzito tayari kwa kusambazwa katika masoko.
Alisema miongoni mwa majukumu ya Wakala ni kuhakikisha vipimo vyote vinavyotumika kwenye biashara na huduma mbalimbali kama vile afya, usalama na mazingira.
Pastory alisema majukumu mengine ya wakala ni kukagua bidhaa zilizofungashwa ku toka nje ya nchi na zile zinazozalishwa hapa nchini na kusimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa njia ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Alitaja jukumu lingine kuwa ni kuidhinisha aina mpya ya vipimo vinavyoagizwa toka nje ya nchi na vinavyoundwa hapa nchini.
More Stories
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam