Na Mohamed Saif, Mwanza
WADAU wa mabwawa kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi wamekutana jijini Mwanza katika warsha ya siku mbili kuhusu miongozo ya usalama wa mabwawa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa kutoka Wizara ya Maji, Domina Msonge amesema, warsha imelenga kujadili na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazoathiri usalama wa mabwabwa.
Amesema, warsha hiyo ni fursa ya kipekee kwa washiriki kujifunza na kuongeza ujuzi na uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa mabwawa ili kulinda rasilimali za maji.
“Tunao wataalam hapa ambao watatupitisha kwenye masuala mbalimbali ya usalama wa mabwabwa kuanzia sheria, miongozo, masuala ya kitaalam na changamoto tunazokutana nazo kwenye utekelezaji wa majukumu yetu,”amesema Msonge.
Msonge aliwasisitiza washiriki watumie fursa hiyo kujadili kwa kina na kutoa michango yao ya hoja zinazojikita katika kusimamia usalama wa mabwawa.
“Ni matarajio yetu kutakuwa na hoja za ufafanuzi, hoja ya kupeana ujuzi zaidi na mwisho wa siku, Rasilimali za Maji zitakuwa salama na hili ndio lengo makhsus la warsha hii,” amesisitiza Msonge.
Aidha, amepongeza ushirikiano unaotolewa na wadau kwenye suala zima la usalama wa mabwawa kuanzia kwa wamiliki wa mabwawa, wadhibiti na wataalam wa mabwawa.
Warsha hiyo inashirikisha viongozi kutoka Wizara ya Maji, wawakilishi kutoka taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), wizara na taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.
Warsha hiyo ya siku mbili inafanyikia katika ukumbi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria jijini Mwanza ilianza leo na itamalizika kesho.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi