May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Wawekezaji jijini Dodoma

Neema ya ardhi yawashukia Wawekezaji

Na Munir Shemweta, Dodoma

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameshusha neema kwa wawekezaji 15 wa makampuni ya ndani na nje kwa kuwapatia ardhi kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali.

Hafla maalum ya kukabidhi hatimiliki na ankara za malipo kwa ajili ya kupatiwa maeneo ya uwekezaji ilifanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa ambao uwekezaji unaenda kufanyika. Mikoa hiyo ni Morogoro, Pwani, Kigoma na Lindi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo (wa pili kulia) pamoja na viongozi wa makampuni ya uwekezaji jijini Dodoma wakati wa kukabidhi Ankara na Hatimiliki za ardhi kwa Makampuni yaliyopatiwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Lukuvi amesema, wizara yake imechukua uamuzi wa haraka wa kuwapatia wawekezaji ardhi ikiwa ni kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutaka wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini wasizungushwe.

‘’Tanzania ni salama anayetaka kuja kuwekeza aje na hakuna suala la kuzungushana na kama itatokea hivyo basi mnitumie ujumbe kuwa kuna mtu anawazungusha, nitachukua hatua,’’alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliiagiza Kamati ya Taifa ya Ugawaji Ardhi kuhakikisha maombi kwa ajili ya kupatiwa ardhi yasizidi wiki mbili na kuitaka kamati hiyo kukaa kila wiki kupitia maombi ya waombaji wote wa ardhi za uwekezaji ardhi kwa haraka.

‘’Sababu zinazobabisha uwekezaji uende taratibu lazima tuziondoe, within seven day mwekezaji lazima apate majibu na kama ni ankara lazima itolewe, hakuna jambo linaloshindikana katika nchi hii,”amesema Waziri Lukuvi.

Kutokana na maombi mbalimbali yaliyowasilishwa tarehe 30 Machi, 2021 kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi kilikaa na kupitisha jumla ya maombi mbalimbali kwa wawekezaji raia na wasiokuwa raia ambapo wawekezaji 15 maombi yao ya kumilikishwa yalipata kibali.

Sehemu ya wawaikilishi wa makampuni ya uwekezaji wakifautilia hotuba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (Hayupo pichani) jijini Dodoma wakati wa kukabidhi Ankara za Malipo na hati kwa wawekezaji walioomba kupatiwa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya Makampuni yaliyopatiwa ardhi ni Pan Tanzania Agriculture Development Limited inayojishughulisha na kilimo cha muhogo na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mihogo, Morogoro Sugar Industries Limited- kilimo cha kisasa cha miwa, Kom Group of Companies Limited uwekezaji kiwanda cha kuchakata nyama ya kuku, kufuga na kutengeneza chakula cha mifugo pamoja na Kampuni ya Kamaka Co. LTD itakayokuwa na ukanda Maalum wa Viwanda.

Waziri Lukuvi amewataka wawekezaji waliokubaliwa maombi yao kuitumia ardhi waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa na kubainisha kuwa wizara yake itafanya ukaguzi kwa ardhi yote iliyotolewa kwa wawekezaji ili kujua kilichofanyika kwa kuwa baadhi yao hawaitumiia kama walivyoomba.

Kwa mujibu wa Lukuvi, inachotaka serikali ni ardhi kuendelezwa ili ipate kodi na wakati huo wananchi wake wapate ajira na kuwataka wawekezaji kuhakikisha wanapopata matatizo kuhusiana na uwekezaji katika sekta ya ardhi basi wawasilishe kwa wakuu wa mikoa wa maeneo husika.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula aliwataka wawekezaji waliopatiwa ardhi kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya kodi ambayo wakati mwingine huwafanya kuona mzigo mkubwa wakati wa kulipa.

‘’Mzingatie sheria katika uwekezaji wenu na mhakikishe mnalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati, mfano mwekezaji mwanzo kodi ya pango la ardhi ataiona kidogo kama 213,000/-lakini akiilaza miaka miwili au mitatu ataona ni ghrama kubwa,”amesema Dkt.Mabula.

Mwakilishi wa Kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Development Limited, Rayson Elijah Luka alisema, kampuni yake itawekeza katika kilimo cha mihogo pamoja na kiwanda cha kuchakata mihogo wilayani Kilwa mkoa wa Lindi na kubainisha kuwa, uamuzi wa kuwekeza eneo hilo unatokana na mahitaji ya muhogo nchini China na uwekezaji huo unatarajia kugharimu takriban dola bilioni 10.

‘’Uwekezaji katika mradi huu wa zao la muhogo utakuwa ni wa kilimo cha kisasa na utatoa ajira rasmi na zisizo rasmi 60,000 katika kipindi cha miaka kumi na katika awamu ya kwanza kutakuwa na ajira 1000. Pia kupitia mradi huo mihogo itabadilishwa kuwa vifungashio ambavyo vikiwekwa kwenye maji vinayeyuka,’’alisema Luka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo aliishukuru Wizara ya Ardhi kwa kukubali maombi ya wawekezaji kupatiwa ardhi kwenye mkoa wake na mikoa mingine na kuwataka wawekezaji kutohodhi maeneo waliyopewa kwa ajili ya uwekezaji bila kuyafanyia shughuli iliyokusudiwa na kusisitiza kuwa wawekezaji hao wanatakiwa kuwasilisha mpango kazi kwake mapema ndani ya kipindi kifupi.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Sanare alisema, mkoa wake hauna ardhi ya kuwapatia wawekezaji ili kukaa nayo bali wanapatiwa ili kuifanyia kazi iliyokusudiwa kwa kuwa katika mkoa huo kuna mapori mengi ambayo hayatumiki na hivyo kuruhusu uvamizi.

‘’Mkoa wetu wa Morogoro tumeomba kufutwa mashamba 48, mwagikeni mkoa wa Morogoro kuwekeza maana Pwani imejaa,’’alisema Sanare.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika upekuzi katika eneo la viwanda lilipo Barabara ya Pugu na maeneo mengine katika mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kujua matumizi ya uwekezaji uliofanyika ili kubaini waliokiuka matumizi ya maeneo hayo.

‘’Pugu road ni eneo la viwanda na hati zilizotolewa ni kwa ajili ya viwanda, lakini kuna maeneo yamegeuzwa kuwa makazi. Maeneo ya viwanda lazima yabaki hivyo na siyo mara Petro station au maduka,’’alisema Waziri Lukuvi.