Na Mwandishi Wetu,timesmajiea, online Sumbawanga
Wizara ya Kilimo imesema imeipongeza Kampuni ya Agricom Africa Limited kwa kupeleka vijijini matrekata na zana nyingine za kisasa za kilimo, kwani zana bora zitawasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi na kuinua kipato cha mkulima.
Akizungumza kwa niaba ya wizara jana wakati wa mafunzo yanayoendelea Wilayani Kalambo, Mkoa Rukwa, Ofisa Mkuu wa Zana za Kilimo wa wizara hiyo, Godwin Mubi, amesema wizara inatambua mchango wa Kampuni ya Agricom katika kuinua na kuboresha kilimo kwa kusambaza zana za kilimo katika maeneo mbali mbali nchini. Mkoa wa Rukwa kwa awamu ya kwanza umetengewa zaidi ya matrekta 17.
Amesema lengo la serikali ni kutumia kilimo kuinua maisha ya wakulima nchini kote. Lakini tatizo ni kwamba wakulima wengi wana uelewa mdogo sana juu ya matumizi ya zana bora na uhusiano wa zana hizo katika kuinua uzalishaji wa mazao na uboreshaji wa maisha yao wenyewe.
“Agricom Africa ni moja wa wadau ambao wamekuwa wakiunga mkono juhudi ya Wizara na Serikali kwa ujumla katika kutekeleza mpango wa kuinua sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) kwa kuhakikisha zana za kisasa zinawafikia wakulima na wanajua matumizi yake.
Tunawapongeza kwa kazi hii inayofanywa kwa manufaa mapana ya taifa letu,” amesema Mubi
Mubi amesema mafunzo yanayoendeshwa na kampuni hiyo yataondoa tatizo la uelewa mdogo wa wakulima juu ya matumizi ya zana za kisasa na kuwafanya wapende kutumia zana hizo.
Amesema matumizi ya zana bora yataongeza uzalishaji mara tatu juu ya uzalishaji unaotokana na jembe la mkono.
“Takwimu zinaonesha matumizi ya trekta kwa mkoa wa Rukwa ni asilimia 4 tu na asiliamia zaidi ya 80 wanatumia wanyama kazi na iliyobaki ni jembe la mkono. Hali hii ndio imefanya mafunzo haya yaanzishwe mkoani Rukwa,” amesema Mubi na kuongeza kwamba Tanzania ina hekta 44 milioni zinazofaa kwa kilimo, lakini ni hekta 10.8 milioni tu ndizo zinalimwa kwa sasa, na kufafanua kwamba hali hii inatokana na matumizi kidogo ya zana bora za kilimo yakiwemo matrekta nchini.
“Ni wakati sahihi sasa kuhakikisha elimu ya matumizi ya zana za kilimo inatolewa kwa wakulima nchini ili kujenga uelewa wa matumizi ya zana hizo jambo litakalosaidia kuongeza eneo la kilimo na kuchochea maendeleo,” amesema Mubi
Mkulima wa Kijiji cha Katete Wilaya ya Kalambo, Monica Mgala, amesema kijiji chao hakina trekta na kusema kwamba kijiji kikipata trekta uzalishaji utaongezeka.
“Kijiji chetu hakina trekta. Tunakodi wanyama kazi kulima mashamba yetu. Na upatikanaji wa wanyamakazi ni taabu kwa sababu ni wachache ukilinganishwa mahitaji,” amesema Mgala
Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Agricom Africa, Philipo William, amewahakikishia wakulima kwamba zana zote zilizopangwa zitawafikia kwa wakati katika msimu huu wa kilimo.
“Zaidi ya matrekta 17 zitakabidhiwa kwa vyama vya ushirika mwezi Oktoba na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Kampuni yetu imejipanga vizuri katika kutoa huduma hiyo muhimu kwa wakulima kwa wakati,” amesema William
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea