January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Kilimo yahamasisha kilimo zao la chikichi Kyela

Na Esther Macha,TimesMajira,Online, Kyela

WIZARA ya Kilimo imeanza kuhamasisha kilimo cha kisasa cha zao la chikichi wilayani Kyela ili kusaidia taifa kujitosheleze kwa mafuta ya kula.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Kyela kwa ajili ya kufuatilia uzalishaji wa mazao ya kimkakati ikiwemo chikichi.

Amesema wanakusudia kuwapelekea wakulima mbegu za kisasa na ni jukumu lao kama wilaya kuwaandaa wakulima ili mbegu hizo zitakapokuwa tayari wazipandwe kwa wingi kwenye mashamba yao.

Amesema mbegu bora za michikichi zinazalishwa mkoani Kigoma na tayari zimeanza kusambazwa maeneo yanayolima zao hilo na kwamba miongoni mwa maeneo ambayo mbegu hizo zitapelekwa ni wilayani Kyela.

Chimagu amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) imeanzisha shamba la mbegu bora za michikichi lililopo wilayani Mbozi ambalo litasaidia upatikanaji wa mbegu hizo kirahisi kwa wakulima wa Kyela.

Katika mwendelezo wa jitihada hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Kituo cha Naliendele cha mkoani Mtwara imeanzisha shamba la mbegu za chikichi lililopo kijiji cha Kikusyab wilayani Kyela kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora.

Chimagu amesema Serikali inao mkakati kabambe wa kuongeza uzalishaji wa zao la Chikichi kwa lengo la kulifanya taifa lijitosheleze kwa mafuta ya kula.

Amesema wilaya ya Kyela ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo wa kuzalisha zao la chikichi kwa wingi, lakini wakulima wamekuwa hawazalishi kwa tija kutokana na kutumia njia za kizamani na mbegu zisizokuwa na ubora.

Ofisa Kilimo Kata ya Itope, Stella Mwakaje, amesema shamba hilo litakuwa ni shamba mama na la mfano kwa ajili ya upatikanaji wa mbegu za kisasa wilayani humo.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo Wilaya ,Kenneth Nzilan, amesema tayari waliandaa shamba lenye ukubwa wa ekari 13 lililopo Kata ya Makwale ambalo litatumika kama shamba darasa ili kuwafundisha wakulima kilimo cha mazao ya chikichi na Cocoa.