May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

????????????????????????????????????

Lukuvi apokea taarifa ya awali mgogoro wa Mtakuja

Na Munir Shemweta,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepokea taarifa ya awali ya uhakiki wa eneo lenye mgogoro la Mtakuja lilipo Kata ya Chang’ombe mkoani Dodoma.

Mkazi wa Mtakuja mkoani Dodoma Stanslaus Barayata (wa tatu kushoto) akihakiki taarifa zake kutoka kwa Afisa Mipango Miji Eliza Lushu (wa pili kulia) wakati wa zoezi la uhakiki wananchi wanaomiliki maeneo yenye mgogoro eneo la Mtakuja lenye ukubwa wa hekta kumi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya wananchi katika eneo hilo Kinara Vangiringa Mwilafi.

Taarifa ya uhakiki wa eneo hilo lenye ukubwa hekta kumi, uliwasilishwa jana katika Ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wilson Luge kwa niaba ya timu inayofanya uhakiki kwa wakazi wanaoishi eneo hilo.

Uwasilishaji wa taarifa hiyo umekuja kutokana na kukwama kwa mara kadhaa mazoezi yaliyofanyika huko nyuma na kusababisha Waziri, William Lukuvi kuelekeza kufanyika uhakiki mwingine ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa muda mrefu kwenye eneo hilo.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi, tayari timu ya uhakiki mgogoro huo imeshawapitia wananchi 750 kati ya 1,025 watakaofanyiwa uhakiki.

Luge amesema, kazi kubwa inayofanywa na timu ya uhakiki ni kupitia taarifa ya kila mwananchi na kuangalia hali ya maendelezo, yaliyofanyika katika kila eneo la mwananchi analomiliki.

Mkazi wa eneo la Mtakuja mkoani Dodoma Janet Charles Mwaluko (Kushoto) akitia saini ikiwa ni ishara ya kukubaliana na uhakiki unaoendelea eneo lenye mgogoro la Mtakuja katika Kata ya Chang’ombe.Mpigapicha Wetu

Amesema mazoezi ya uhakiki eneo la Mtakuja, yamefanyika mara kadhaa katika miaka ya 2005, 2008 na 2015 ambapo zoezi linaloendelea sasa linatarajiwa kuleta suluhu ya mgogoro huo.

Luge amesema uwasilishwaji taarifa ya uhakiki wa mgogoro wa eneo la Mtakuja Dodoma, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, Naibu wake Nocolaus Mkapa, Kamishna wa Ardhi Nathaniel Nhonge na Watendaji wa Wizara, Jiji la Dodoma pamoja na wa Kata ya Chang’ombe.