May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Elimu yatoa wito wadau kupanga mipango ya maendeleo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WIZARA ya Elimu imetoa wito kwa Wadau wa Elimu kushiriki kikamilifu katika kupanga Mipango ya Maendeleo ya Elimu na program mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha elimu inaleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Aprili 4,2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Prof. Carolyne Nombo,kwa niaba ya Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa pamoja wa tathimini wa sekta ya elimu kwa mwaka 2023/24  amesema kuwa Mkutano huu utawawezesha Wadau kujadili changamoto mbalimbali, kuweka mikakati ya  namna ya kukabiliana nazo, kuweka maazimio na mikakati mbalimbali ya Uboreshaji wa Elimu nchini.

Amewataka wadau wote wanaoshiriki katika Mkutano wa mwaka huu wa Tathmini ya Pamoja ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu,watumie fursa hiyo kujadili kwa kina mawasilisho yatakayofanyika na kutoa maoni yenye tija katika kuboresha elimu nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt.Charles Msonde amesema  Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu na kuwa mkutano huo utakuwa ni fursa ya kuangalia hayo na kubainisha changamoto ili kuendelea kuboresha sekta hiyo ambayo ni muhimu katika mendeleo ya nchi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amesema wadau kwa pamoja watajadili changamoto na mafanikio katika sekta ya elimu na hatimaye kuja na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu

“Wizara imefanya mageuzi makubwa kupitia Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na sasa tuna Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na pia Mitaala Mipya ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu.

“Sera ya Elimu na Mitaala ndiyo nyenzo mama katika utoaji Elimu nchini,  na hiwahakikishie uwa zimefanyiwa kazi kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia mazingira yetu na hitaji la soko  na zitawasilishwa kwa kina katika Mkutano huu. “

Aidha amesema kuendeleza Rasilimaliwatu ni moja kati ya majukumu ya msingi yanayotekelezwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana OR – TAMISEMI na Wadau wa Sekta ya Elimu.

“Eneo hili linajumuisha kuandaa na kutekeleza programu na mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimaliwatu nchini, kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajirika ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.”amesisitiza

Mkutano huo unaenda na kaulimbiu ya  Elimu kwa Maendeleo Endelevu inaakisi mwelekeo wa Serikali katika mageuzi makubwa yaliyofanyika pamoja na yanayoendelea kufanyika ili  Elimu iwe chombo cha Kimkakati katika kuleta Maendeleo Endelevu  na kuwawezsha Watanzania kwendana na kasi ya mendeleo katika ulimwengu wa utandawazi .