May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Elimu yaanza utaratibu mpya maadhimisho wiki ya MAKISATU

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  imeanza utaratibu mpya ambapo utakuwa na Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa pamoja.

Ambayo ni matokeo ya kuunganisha yaliyokuwa Maadhimisho ya Kitaifa ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama MAKISATU, Maonesho ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaliyokuwa yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyokuwa yanaratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Aprili 9,2024 na Waziri wa Wizara hiyo Prof.Adolf Mkenda ambapo alitumia fursa hiyo kufungua dirisha la usajili wa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaani MAKISATU.

“Dirisha la usajili limefunguliwa rasmi leo tarehe 9 Aprili 2024 na litafungwa tarehe 08 Mei 2024 na  Mashindano haya yatahusisha wabunifu kutoka Vyuo Vya Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Shule za Msingi, Shule za Sekondari na wabunifu kutoka Mfumo usio rasmi.

“Washindi 10 kwa kila kundi watashiriki katika maadhimisho ya ngazi ya kitaifa na washindi wa jumla wataingia katika mpango wa Serikali wa uendelezaji na ubiasharishaji wa bunifu zao,”amefafanua 

Aidha Prof.Mkenda amesema kuwa  Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.

“Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatazileta pamoja Taasisi, Mashirika, Wadau wa Maendeleo, Asasi, Watunga Sera, Wabunifu/wagunduzi, na Wadau wengine mbalimbali kwa ajili ya mijadala, na kushuhudia tafiti, bunifu na teknolojia zinazozalishwa nchini. 

“Halikadhalika maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wabunifu na watafiti nchini kuonana na wawekezaji wanaoweza kuchangia kwa namna mbalimbali katika kuendeleza na kubiasharisha matokeo ya tafiti na bunifu zao,”amesema.

Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka 2024 yatafanyika Mkoani Tanga kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei 2024 katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Popatlal yanayokwenda na kaulimbiu ya wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Tanzania kwa mwaka 2024 ni “Elimu,Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani ambayo inachagiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu na teknolojia katika maendeleo ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa katika hafla ya ufunguzi atakuwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim  Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya kilele.

Vilevile amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatatanguliwa na matukio katika ngazi za mikoa na halmashauri ikiwemo maonesho ya ubunifu na teknolojia, mikutano na midahalo chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Programu ya FUNGUO-UNDP, Ofisi za Makatibu Tawala Mikoa na wadau wengine.

Ambapo amesema Mwaka huu wanatarajia kuwa na washiriki kutoka taasisi za umma na binafsi zipatazo 339 watakaojumuisha Vyuo Vya Elimu ya Juu na Taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi.