Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipo mbioni kuanza ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Anatoglou kitakachojengwa wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam ambacho kitagharaimu Shilingi milioni 700.
Akiongea hivi karibuni wakati anakagua eneo kitakapojengwa Chuo hicho, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Omary Kipanga ameagiza ujenzi wa chuo hicho kuanza mara moja kwa kuwa fedha za ujenzi huo tayari zipo.
Aidha Mhe. Kipanga ameelekeza wasimamizi wa ujenzi huo kuanza kutekeleza hatua za awali wakati wanasubiria fedha za awali ziingie.
“Mnaweza kuanza kufanya maandalizi ya awali kwa kusafisha eneo, kuunganisha maji na kuunda Kamati za ujenzi ili fedha zikishaingia kazi ianze kwa kasi,” amesema Kipanga.
Kipanga amewataka Wasimamizi wa ujenzi kushirikiana kwa karibu na Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala, Mkurugenzi wa Manispaa na Afisa Ardhi ili kazi iende vizuri na kwa ufanisi.
“Wasimamizi wa ujenzi ntataka kuona mpango kazi kabla hamjaanza ujenzi na pia nawaagiza kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Wilaya ili kazi iweze kwenda vizuri,” amesema Kipanga.
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Noel Mbonde amesema ujenzi wa chuo hicho kitakachokuwa na jumla ya majengo 10 utaanza Oktoba 2021na kwamba unatarajiwa kukamilika Machi, 2022.
Mbonde amesema chuo hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 200 kwa wakati mmoja. Amesema fedha za awali za ujenzi huo, Shilingi milioni 400 zitakabidhiwa hivi karibuni ili ujenzi uweze kuanza mara moja.
Mkuu wa chuo hicho, Victoria Isundwa amesema chuo kwa sasa kinatumia majengo ya Manispaa ya Ilala iliyopo Mnazimmoja, Dar es Salaam na kwamba kina jumla ya wanafunzi 68 wanaosoma kozi za upishi na ujenzi, kati yao 38 ni wenye taahira ya akili.
Amesema ujenzi utakapokamilika chuo hicho kitatoa kozi katika fani ya useremala, ushonaji, uchomeleaji vyuma, ufundi magari, kilimo na ufugaji.
Isundwa amesema chuo kina eneo la ekari 14.5 na ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuwajengea majengo ya chuo na kuongeza kuwa anaamini wataweza kutoa mafunzo kwa ufanisi zaidi wakiwa kwenye eneo lenye nafasi ya kutosha.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi