Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
WAZIRI wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali ya za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amesema ni vema jamii ya Watanzania ikiendelea kutunza mazingira kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa na athari nyingi.
Ameyasema hayo wakati wa utoaji tuzo kwa washindi 10 wa shindano la Mazingira Yangu Wajibu Wangu lililoandaliwa na Taasisi ya FEET.
Hafla hiyo imefanyika Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Liberata Mulamula na Balozi wa Ufaransa nchini Fr’ederic Clavier.
Amesema mazingira ni maisha, uchumi, nishati, afya na ndio kila kitu hivyo amesisitiza ni vema kila mmoja mwananchi akatambua anao wajibu wa kutunza mazingira yanayomzunguka.
“Na kwa hali hiyo wote tunawajibu wa kutunza, kulinda na kuhifadhi mazingira yetu”.
Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wadau wanaoshiriki kutunza mazingira kwa kupanda miti ikiwemo taasisi ya FEET ambayo imejipanga kupanda miti 1000 huku akieleza kuwa wanataka kuviwezesha vijiji kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa kuanisha maeneo kulingana na mahitaji.
“Kwa hiyo tunataka kila kijiji Tanzania tuseme hapa ni kwa ajili ya mifugo, hapa kilimo , au tunataka kuwa na makazi ni jambo ambalo tutalifanya na lengo ni kuhakikisha tunatunza mazingira yetu.
Nawapongeza FEET kwa kujikita kwenye utunzaji mazingira na nimefurahi kuona vijana wakiwa mstari wa mbele kutunza mazingira na tunapaswa kutambua Mazingira yangu wajibu wangu,”amesema.
Aidha ameshukuru Balozi Clavier kwa utayari wake wa kushirikiana na TAMISEMI katika kutunza na kuhifadhi mazingira pamoja na masuala ya jinsia katika upande wa usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki Liberata Mulamula amesema amesema amefurahishwa na jitihada za vijana kupitia taasisi ya FEET kutambua suala la utunzaji mazingira ni la sote, hivyo amesisitiza umuhimu wa mazingira kutunza huku akieleza huko nyuma sehemu kubwa ya Tanzania ilikiwa kijani lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya, ile rangi ya kijani imepungua.
“Kuhusu hali mbaya ya mazingira mimi natoka Mkoa wa Kagera ambao ulikuwa mkoa mzuri kwa maana ya hali ya kijani iliyotokana na uwepo wa mazingira asilia, lakini sasa hivi ukienda hakuna,”amesema Waziri Mulamula, huku akitumia nafasi hiyo kuihamaisha jamii kutunza mazingira.
Wakati huo huo Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi huku akifafanua nchi yao imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na nchi za Bara la Afrika kuhakikisha mazingira yanatunzwa.
“Ufaransa inataka kuwa mshirika wa karibu zaidi katika umoja wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwa kusaidia mipango ya ndani. Tumekuwa tukishiriki kwa haua mbalimbali na tutaendelea,”amesema Balozi Clavier.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya FEET Lubango Kitwanga amesema ni vema vijana ni vema wakashiriki kikamilifu kutunza mazingira na mazingira ni yale ambayo yanamzunguka kila mtu huku akifafanua shindano ambalo walikuwa wameliandaa kijana alitakiwa kupiga picha ya mazingira yanayomzunguka na kisha kuelezea atafanya nini kuhakikisha anashiriki kuyatunza.
“Tunawashukuru wote ambao wameshiriki kwenye tukio hili la kutoa tuzo kwa washindi lakini na kushuhudia maonesho ya picha zinazoonesha uharibifu wa mazingira.FEET pamoja na mambo mengine tutapanda miti 1000 kuanzia Juni 26 mwaka huu.
“Tunaomba watu wajitokeze na kupenda mazingira yao, kumalizika kwa shindano hilo sio mwisho wa kutunza mazingira , bado tutaendelea kupokea picha za mazingira ili tuendelee kubadilisha.FEET mchango wetu kwenye jamii tumeakua kuja na kampeni inayosemwa Mazingira Yangu , Wajibu Wangu tukiwa na maana ya kuhamasisha utunzaji mazingira,”amesisitiza Kitwanga.
Wakati huo huo washindi wa tuzo hiyo Rebeca Muna na Godfrey Haule wamesema waliamua kushiriki shindano hilo kwa kutambua umuhimu wa vijana kushiriki kwenye kutunza mazingira kwani ni wajibu wa kila mtu kutunza mazingira yanayomzunguka.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba