May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuimarish ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Na Joyce Kasiki, TimesMajira,Online Dodoma

WAZIRI wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kuna kila sababu ya kuimarishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kuiondolea Serikali mzigo wa gharama kubwa kwa ajili ya kuwalipa mawakili wa nje ya nchi katika kwa ajili ya kusimamia mashauri yanayoikabili serikali nje ya nchi.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa watumishi wa ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini hapa, Profesa Labudi amesema,kuimarishwa kwa ofisi hiyo pia kutaleta tija katika mashauri ya ndani ya nchi ambayo yanasimamiwa na mawakili wa Serikali.

“Kuna kila sababu ya ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali, kwani ina majukumu mengi hasa ya kusimamia mashauri yanayoikabili Serikali ndani na nje ya nchi na hii itaiondolea Serikali gharama kubwa ambazo imekuwa ikitumia kulipa mawakili wa nje ya nchi kutokana na uwezo walio nao,” amesema profesa Kabudi

“Hawa viongozi wetu Mama Samia ( Rais Suluhu Hassan) hata wakati ule wa Hayati John Magufuli wanapata shida sana unakuta wametenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye miundombinu au miradi ya maendeleo, lakini unakuta nchi inashitakiwa na kwenda mahakamani unatakiwa kutumia fedha nyingi sana kulipa mawakili,”amesema Prof. Kabudi

Amesema kitendo cha kutumia mawakili wa nje ya nchi wakati serikali inaposhitakiwa nje kunasababish Serikali kutumia fedha ambazo zilikuwa zitumike kwenye shughuli nyingine za maendeleo na hivyo kukwamish shughuli husika.

“Lakini tukiwa na mawakili wetu ambao wana uwezo wa kusimamia mashuri yote ya ndani na nje ya nchi,wataenda kusimamia mashauri hayo na hivyo kupunguza gharama hizo,” amesisitiza

Aidha amesema,ipo haja ya Taifa kuwa na taasisi za Serikali za kutoa mafunzo ili kila baada ya muda iwe inatoa mafunzo kwa mawakili ili kuwajengea uwezo wa kusimamia mashauri hayo.

“Lazima kama nchi tuanze kufikiria kuwa taasisi za Serikali za mafunzo ili kila baada ya muda mawakili hawa wapate mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu mpya za kuyakabili mashauri ya serikali ya ndani na nje ya nchi ” amesema Prof Kabudi na kuongeza;

“Na huko baadaye itabidi suala la mafunzo tulifanye kama hitaji la kisheria kwamba kila wakili lazima aende mafunzo lengo lake kubwa ni kutaka kuboresha utendaji wa mawakili wetu ambao utasaidia kuokoa fedha nyingi zaidi za Serikali .”

Vile vile amewataka mawakili hao kuwa makini katika matumizi ya lugha za kiswahili na kingereza mahakamani.

“Matumizi ya lugha ya kiswahili mahakamani yameanza ,tushirikiane kwa pamoja tuanze kuona namna gani tunakuwa na lugha moja,”amesema.

Awali ,Wakili Mkuu wa serikali Gabriel Malata ameelezea changamoto zinazoikabili ofisi hiyo kuwa ni pamoja na uhaba wa watumishi pamoja na ukosefu wa vitendea kazi yakiwemo magari.