October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Sangu aipongeza WCF na TRC

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amepongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana katika ujenzi wa miradi ya kimkakati ambayo imekuwa na tija katika kukuza maendeleo ya Taifa.

Aidha, amezitaka sekta nyingine za Serikali na binafsi kuiga taasisi hizo katika kuendeleza vitega uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

Sangu ameyasema hayo leo, Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa ujenzi wa kumbi za mikutano na hoteli ya nyota nne kati ya WCF na TRC, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Stesheni ya SGR Jakaya Mrisho Kikwete, mkoani Morogoro.

Amesema, katika makubaliano hayo kumbi za mikutano 26 zenye uwezo wa kuhudumia watu kuanzia 10 hadi 600, kulingana na mahitaji, pamoja na hoteli ya nyota nne yenye vyumba takribani 91 katika eneo la Stesheni ya SGR Jakaya Mrisho Kikwete.

Ujenzi huo unakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 65 na ni miongoni mwa fursa za uwekezaji zinazoambatana na mabadiliko ya Sheria ya Reli ya mwaka 2017, iliyofanyiwa maboresho mwaka 2023, inayoruhusu uwekezaji katika maeneo ya reli ili kuendeleza sekta ya reli na kujenga uchumi imara wa nchi kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Vilevile, Sangu amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya katika kushirikisha sekta mbalimbali za Serikali katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa vijana.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema kuwa uendelezaji wa miundombinu ya reli nchini utaendelea kuleta mabadiliko katika maeneo mbalimbali ya nchi na kufungua fursa za kiuchumi, huku akiwataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza.

Mhe. Kihenzile ameahidi kuwa licha ya Serikali kujenga reli kwa ajili ya kusafirisha mizigo na abiria, itajikita kuhakikisha TRC inatumia rasilimali ilizonazo kwa kushirikiana na mashirika mengine kufungua fursa za uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa majengo ya biashara, kilimo, utalii, viwanda na kadhalika.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Renatha Rugarabamu, amesema WCF imeamua kuwekeza ikiwa ni utekelezaji wa sheria inayoyataka mashirika kuwa na vyanzo vya mapato vitakavyoyawezesha kujitegemea.

“Wote mnajua sisi WCF huwa tunalipa waathirika wa maeneo ya kazi. Sasa ili tuweze kuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wanachama wetu, tumeona ni vyema tuwe na vitega uchumi ili kusustain malipo kwa wanachama wetu ambao wanahitaji malipo ya muda mrefu,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF),Renatha Rugarabamu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Jaffer Machano, amesema ujenzi wa kumbi za mikutano na hoteli ya nyota nne utakaofanywa na WCF umekuja wakati sahihi, ikizingatiwa kuwa kwa siku TRC inasafirisha abiria zaidi ya 2,800 kutoka Dar es Salaam na Morogoro.