October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikwazo visiwakatishe tamaa:Joshua Mwakanolo

Na Mwandishi wetu ,TimesmajiraOnline,Mbeya

Mwanzilishi wa kampeni ya Nisome, Joshua Edward, amewataka vijana kutokata tamaa katika kupambania ndoto zao kutokana na vikwazo wanavyokutana navyo, badala yake wajifunze kutoka kwa watu waliofanikiwa katika ndoto na maeneo wanayolenga kufikia.

Joshua amesema hayo wakati wa kuwafanyia mafunzo viongozi wa mitaa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwahamasisha vijana kuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu, akieleza kuwa vitabu ni chanzo muhimu cha maarifa yanayoweza kuwasaidia vijana kuongeza ujuzi na uelewa.

Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa ya kujisomea vitabu kama njia mojawapo ya kujenga uwezo wao na kupata maarifa yatakayowasaidia katika kufikia malengo yao ya maisha, pamoja na kujifunza uzoefu wa watu waliofanikiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ilindi, Kata ya Ilemi, Mkoa wa Mbeya, Abdul Kilasi, amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa viongozi na jamii kwa ujumla, hususan vijana.

Kilasi amesema kupitia mafunzo hayo wamepata uelewa kuhusu masuala ya uchumi na namna vijana wanavyoweza kujenga uwezo wao ili kufikia ndoto walizojiwekea katika maisha yao binafsi.

“Mafunzo haya yatakuwa msaada mkubwa kuhusu uchumi na yataweza kuwafumbua macho baadhi ya vijana wetu ,tunaamini yamekuja muda mwafaka yatawajenga “amesema.