December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nishati mbadala kuhifadhi mazingira

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesisisitiza wananchi kutumia nishati mbadala ili kuhifadhi na kutunza mazingira kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi

Nahodha Mwandamizi kutoka Idara ya Uvuvi Bw. Dickson Stowa akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Mashimba Ndaki juu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa kutumia Zana za Uvuvi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre, Dodoma

Waziri Ndaki ameyasema hayo alipotembelea baadhi ya mabanda kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliyofanyika Katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convetion Centre ,Jijini Dodoma na kusisitiza elimu zaid juu ya nishati mbadala Kwa Wananchi ili kutunza Mazingira vizuri.

“Tujali sana kutunza mazingira tunapofanya shughuli za kiuchumi na kijamii, kwenye shughuli za kufuga na kuvua lazima tujali kuhifadhi mazingira, tusipohifadhi mazingira tutakosa na mazalia ya samaki na samaki watakosa chakula”amesema Waziri Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akipatiwa maelezo ya namna ya kuandaa udongo wa kuoteshea miche kwa ajili ya kutunza Mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa mradi wa “The Young World Feeders” Bw. Ray Peter

Ndaki amesema kuwa ili shughuli zetu za ufugaji na uvuvi ziweze kuendelea tuhifadhi kwenye maeneo ya nchi kavu, bahari , mito, maziwa na maeneo ya misitu ili ziweze kuwa endelevu.

“Watanzania tutunze mazingira ya nchi yetu ili yaweze kututunza”alimalizia Waziri Ndaki alipokuwa akihitimisha wito wake kwa Wananchi .

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani (Sekta ya Mifugo) Dkt. Kejeri Gillah amesema kuwa, wafugaji wazingatie namna bora ya kufuga mifugo yao, kuhifadhi na kutunza mazingira vizuri.

“Kabla ya kupanda malisho ni vizuri kujua mbegu inayostahimili ikolojia na wafugaji wazingatie malisho yanayostahimili katika maeneo husika”, alisema Dkt. Gillah.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akipewa elimu na Mratibu wa Miradi ya Uhifadhi wa Wanyama Pori Bw. Rich Katondo juu ya Wananchi kujikinga na mazao yao ili Kupunguza migogoro kati ya Hifadhi ya wanayama pori na mifugo

Aidha,DktGilla amebainisha kuwa watu wanapochinja Mifugo yao takataka zinazotokana na Mifugo hiyo inaenda kuchafua mazingira, hivyo tunashauri wafugaji kuzingatia namna bora ya kutunza Mifugo na mazingira.

Naye Mkuu wa kitengo cha mazingira (Sekta ya uvuvi) Bw. Melton Kalinga, amesema kuwa lengo la maonesho haya ni kutumia zana za uvuvi rafiki kwa mazingira kwa ajili ya kutunza viumbe hai majini, hususani samaki.

Aidha,Nahodha Mwandamizi kutoka Idara ya Uvuvi Dickson Stoah ameongeza kuwa, uharibifu wa mazingira unatokana na Utumiaji wa zana haramu majini na hivyo kuathiri mfumo mzima wa viumbe maji.

Kwa upande wa Wadau wa mazingira waliokuwa wanatembelea mabanda, baadhi ya washiriki wameipongeza Serikali kwa kuweka Maadhimisho hayo kwa ajili ya kuelimisha na kujifunza juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati mbadala kuongoa mfumo wa ikolojia.