December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Makamba ataja maeneo ya kuboresha Wizara ya mambo ya nje

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba ametumia takribani saa moja kuelezea maeneo ambayo yatajajadiliwa katika warsha ya Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani inayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha kuanzia tarehe 21 hadi 24 Aprili 2024.

Waziri Makamba amewataka washiriki wa warsha hiyo ambao ni Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wakuu wa Utawala balozini, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Wizara hiyo kujadili kwa upana maeneo hayo ili Wizara iweze kufikia malengo iliyowekewa na Serikali.

Maeneo ambayo ameyataja, Mhe. Waziri ni pamoja na kuboresha mawasiliano ndani ya Wizara, baina ya Wizara na taasisi nyingine na wadau wake.

Amesema hakuna namna Wizara ambayo majukumu yake ni uratibu ikafikia ufanisi unaohitajika bila kuwa na mfumo madhubuti wa mawasiliano.

Amesema eneo lingine ni umuhimu wa Wizara kuweka mfumo madhubuti zaidi wa kufuatilia utekelezaji wa matukio ambayo imekuwa ikiyaratibu tena kwa ufanisi mkubwa.

Matukio hayo ni pamoja na masuala yanayoafikiwa katika ziara za viongozi, Mikutano, makongamano ambayo yana faida kubwa kwa nchi kama yatafuatiliwa vyema utekelezaji wake .

Mhe. Waziri aliongeza kuwa kuna umuhimu wa Wizara wa kuweka
mfumo wa kuwaongezea maarifa, weledi na ujuzi maafisa wake, hususan katika uandishi na kuzungumza.

Amebainisha kuwa nchi yetu inasifika na kutangazika kutokana umahiri wa wanadiplomasia wake, jambo ambalo
limekuwa ni kama urithi wetu, hivyo lazima jambo hili liendelezwe kwa kuwapatia watumishi ujuzi unaohitajika.

Suala lingine ambalo Mhe. Waziri amelisisitiza ni umuhimu wa kuwa na mfumo wa kuwajibishana. Amesema mfumo huo utasaidia kuhamasisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika Wizara.

Alisisitiza pia umuhimu wa
kuendelea kulinda heshima na hadhi ya nchi yetu huko Nje.

Alisema kuwa kufanikisha hilo ni pamoja na kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi huko nje ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea kazi vinavyohitajika.

Alisema Serikali itahakikisha inaboresha mazingira ya kazi ili nchi iendelee kulinda heshima yake iliyojengwa kwa muda mrefu na viongozi waliopita.

Mhe. Waziri alihitimisha mazurngumzo yake kwa kuwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Amesema tokea ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda wa miezi saba sasa amebaini kuna uwezekano wa kufanya mambo makubwa zaidi na ndiyo moja ya sababu ya kuitisha warsha hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ya kubainisha changamoto, kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mpango wa utekelezaji wenye tija kwa maslahi ya nchi.