Na Joyce Kasiki, TimesMajira,Online Chita
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa kwa mara
ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, ametembelea skimu ya
umwagiliaji ya zao la mpunga katika kikosi 837 Chita JKT Ifakara
mkoani Morogoro kujionea shughuli zinazofanyika katika kikosi hicho,
huku akiahidi kuendeleza kazi hizo kwa maslahi mapana ya wananchi na
Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwenye ziara hiyo Kwandikwa amesema mradi huo ni miongoni
mwa miradi mingi inayotekelezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika vikosi vyake nchini ambavyo vimejiwekea lengo la kujitosheleza kwa chakula.
“Miradi hii nilikuwa naisoma tu kwenye makarasi na nilisema nikipata
muda nitaitembelea na leo hii nimekuja kujionea kwa macho nini
kinafanyika hapa, kimsingi nimefurahi kukuta shughuli zinazoendelea
hapa ambazo hata mimi mwenyewe nimejifunza kitu ambacho hata wanancjhi
wangu wa Ushetu (jimboni) wanapaswa kupata elimu hii.”amesema na
kuongeza kuwa
“Ukiacha skimu hii ya umwagiliaji kuna mradi wa ufugaji samaki,ambao
kama mnavyoona mabwawa yamejengwa kwa teknolojia rahisi na yenye gharama
nafuu kabisa ambazo ni rahisi hata kwa wananchi kumudu ujenzi wake.”
Kutokana na kuridhishwa na utekelezwaji wa mradi huo, Kwandikwa amesema
Wizara yake itahakikisha inafanya uwezeshaji ili miradi hii isonge
mbele zaidi.
“Niseme tu nimeridhishwa na miradi inayotekelezwa hapa, nimeona ujenzi
wa ghala,lakini pia tuna ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mpunga pamoja
na ufugaji wa samaki na tukikamilisha mradi huu tutakwenda kulima
ekari 12,000 sio jambo dogo,”amesisitiza Waziri huyo
Aidha amesema mradi wa kilimo cha mpunga ambao pia umejikita katika
uzalishaji wa mbegu unakwenda kuwasaidia wananchi kwa kuwa na
upatikanaji wa mbegu bora za uhakika.
“Tayari kuna shamba la mbegu bora ya mpunga aina saro five ,na
nimeambiwa na wataalam kwamba hii ndio mbegu bora zaidi katika kilimo
cha mpunga kwa hiyo wakulima watarajie muda si mrefu sana tutakwenda
kuzalisha mbegu bora za mpunga, na tutaendelea kufanya utafiti na
uzalishaji wa mbegu kwa ajili ya maeneo mbalimbali katika vikosi vyetu
ili kupunguza adha kwa wananchi ya upatikanaji wa mbegu bora.”amesema
Kuhusu mradi wa ufugaji samaki Waziri huyo, amesema mradi huo
utasaidia vijana wa JKT kupata elimu na kuelimisha jamii kuhusu mradi
huo ambao unatekelezwa kwa gharama za chini lakini pia wananchi
watapata chakula bora.
“Hawa vijana waliopo hapa wanaendelea kupata elimu ya kutosha
kutengeneza miundombinu ya ufugaji wa samaki lakini pia kwenda kueneza
elimu, uzoefu wao natarajia wataenda kutoa elimu yenye tija baada ya
kumaliza mkataba wao hapa.”amesema
Waziri Kwandikwa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa maeneo
mbalimbali kwenda kujifunza shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanyika
katika kikosi hicho ili nao waweze kuzalisha kwa tija.
“Watanzania waone namna tunavyozalisha kwa tija,ukizalisha samaki
hapa una fursa ya kuuza nje ya nchi na ahadi yangu kama msimamizi wa
Wizara, Wizara itaendelea kuweka nguvu kubwa kuhakikisha miradi hii
inakuwa na tija,”amesisistiza Waziri Kwandikwa
Naye Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Rajab Mabele
amesema mradi huo ulianza chini ya mtangulizi wake Meja Jenerali
Charles Mbuge, huku akisema anaendeleza kazi hizo na kwamba lengo ni
kuhakikisha JKT linajitegemea kwa chakula ifikapo mwaka 2024/25.
“Vikosi vyetu kote nchini vinatekeleza miradi ya Kilimo cha mazao tofauti tofauti ambayo yote kwa pamoja imelenga kujitosheleza kwa chakuka,kwa hiyo utaona kila kikosi kina shughuli inayofanyika ambapo vikosi vitajilisha kwa kubadilishana mazao..,kwa hiyo mchele unaozalishwa Chita utaenda kwenye vikosi vingine, lakini na chita nao watapata mazao mengine kama mahindi ambayo huzalishwa kwenye vikosi vingine.” Amesema Brigedia Jenerali Mabele
Akitoa taarifa ya miradi inayofanywa na JKT Kikosini hapo Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT Kanali Hassan Mabena amesema ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya kilimo cha mpunga ulianza Julai mwaka 2020 baada ya Jeshi hilo kuna na Mkakati wa Kilimo uliolenga kujitosheleza kwa chakula ifikapo 2024/25 na kwamba mradi ulilenga kulima mara mbili
kwa mwaka yaan masika na kiangazi.
Aidha amesema katika msimu wa kilimo uliopita walikuwa wamejiwekea
lengo la kulima ekari 2,500 lakini wamevuka lengo hilo na kulima ekari
2,700 na tayari wamevuna ekari 650 ambayo yamepatikana magunia 6,720
sawa na wastani wa gunia 10 hadi 11 kwa ekari moja.
Kanali Mabena ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kilimo Mkakati ,mifugo na uvuvi wa JKT, amesema baada ya kukamilika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji
watazalisha chakula kingi zaidi na hatimaye Jeshi hilo litaipunguzia
Serikali gharama za kuwahudumia vijana hasa kwa upande wa chakula.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee