May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Jafo:Ukusanyaji mapato kwa kielektroniki umeleta mafanikio

Na Joyce Kasiki,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI ) Selamani Jafo amesema,ukusanyaji wa mapato kupitia mifumoya kielektroniki ni miongoni mwa mafanikio ya Ofisi yake kwa kipindi cha miaka mitano chini Rais John Magufuli ,kwa kuwezesha kukusanywa kwa mapato kwa zaidi ya asilimia 94 tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kutimika kwa mifumo hiyo ya kukusanyia mapato ambapo Halmashauri zilikusanya chini ya asilimia 70.

Jafo alitoa kauli hiyo leo jijini hapa wakati akizungumza katika siku ya tatu ya Tamisemi Idara ya Miundombinu ambayo imeongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Miundombinu bora katika Tamisemi ni nguzo muhimu
katika uimarishaji wa uchumi wa kati.

Waziri huyo amesema,kipindi hicho idara ya Tehama imefanya kazi kubwa sana ambapo kutokana na mifumo hiyo ya kisasa iliyopo imewezesha hata uandaaji wa bajeti kutumia muda mchache Zaidi.

“Tamisemi inaongoza katika mifumo ya kisasa zaidi ,kabla ya mifumo hii halmashauri zilikusanya fedha kidogo tofauti na ilivyo sasa ,lakini pia watumishi wa Halmashauri walikuwa wakiandaa bajeti kwa miezi miwili lakini sasa ndani ya wiki kazi hiyo inakuwa imekamilika,haya ni mafanikio makubwa sana ,”amesema Jafo.

Pia amesema,katika eneo la huduma za afya, hospitali za wilaya zilikuwa zinakusanya shilingi milioni nne lakini sasa ,kwa kutumia mifumo hiyo zinakusanya shilingi milioni 40 kwa mwezi.

Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara na majengo katika kipindi cha Novemba 2015 hadi Julai 2020 ,Ofisi ya Rais Tamisemi imetumia kiasi cha shilingi trilioni 1.186 kutoka mfuko wa barabara kwa ajili ya matengenezo,ukarabati na ujenzi wa barabara na madaraja .

“Katika kipindi hicho Tamisemi imetumia jumla ya shilingi 1.080 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 133.192.77 ,madaraja 250,makalvati 3,361 na mifereji yenye urefu wa kilomita 67.766 sawa na wastani wa matengenezo ya kilomita 26,638.55,madaraja 50 ,makalvati 672 na mifereji urefu wa kilomita 14 kwa mwaka .”alisema Jafo.

Aidha amesema jumla ya shilingi bilioni 106.451 zimetumika katika ujenzi na ukarabati wa barabara za lami urefu wa kilomita 136.95 barabara za changarawe urefu wa kilomita 1,092 .63 ,barabaa za mawe kilomita 3.5 na madaraja 75.

Waziri huyo amesema,Serikali imefanya kazi kubwa ya kutengeza miundombinu mingi ikiwemo ofisi za wakuu wa mikoa ,ofisi wa wakuu wa wilaya,ofisi za wakurugenzi ,nyumba pamoja na miundombinu hiyo ya barabara.

Hata hivyo alishangazwa na baadhi wananchi ambao wamekuwa wakitumia baadhi ya miundombinu hiyo vibaya ikiwemo miundopmbinu ya barabara kwa kupitisha mfugo kama ng’ombe ambao wamekuwa wakiiharibu ndani ya
kipindi cha muda mfupi.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kwa ujumla kuhakikisha miundombinu yote inayojengwa nchini kuhakikisha wanaitunza ili itumike kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.