January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa kufunga mashindano UMISAVUTA 2021

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Mtwara

WAZIRI wa Michezo Sanaa na Utamaduni, Innocent Bashungwa,anatarajiwa kufunga rasmi mashindano ya kitaifa ya Umoja wa michezo na sanaa vyuo vya elimu Tanzania(UMISAVUTA) kwa mwaka 2021,kwa kukabidhi medali kwa bingwa wa soka wa mashindano hayo kwenye mchezo utakaochezwa kesho katika uwanja wa Nangwana Sijaona mkoani Mtwara kati ya Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini.

Washiriki wa mashindano ya ngoma kuroka kanda ya Kaskazini

Katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,pia Bashungwa atakabidhi medali kwa bingwa wa soka wa michuano na atashuhudia burudani kutoka kwa washindi wa jumla wa kwaya,ngoma za asili na maigizo ambayo ni sehemu ya michezo iliyoshindanishwa tokea kuanza kwa mashindano hayo ya Umisavuta Novemba 29 mwaka huu

Mwenyekiti wa kitaifa wa mashindano ya UMISAVUTA,Doroth Mhaiki amesema wakati akikabidhi medali kwa washindi mbali mbali katika mashindano ya kukimbia kwa umbali tofauti .

Amesema kutokana na mashindano hayo ya UMISAVUTA wamepata vipaji mbali mbali katika michezo tofauti hali inayoawafanya wawe na uhakika wa kushinda katika mashindano ypyote yatakayoshirikisha vyuo tofauti nchini.

“Naibu Waziri wa Michezo sanaa na Utamaduni Pauline Gekul,alitufungulia mashindano haya Novemba 29 mwaka huu na sasa waziri Bashungwa atakuja kuyafunga,kwa kushuhudia mchezo wa soka kati ya kanda ya mashariki na Kanda ya Kaskazini, baada ya kanda zingine tano kushindwa kufikia hatua hiyo kwenye soka”amesema Mhaiki.

Amesema katika mashindano hayo changamoto kuu watakayoondoka nayo ni pamoja na kukosekana kwa viwanja bora vya kufanyia michezo tofauti,muda na idadi ya washiriki na kusema wataenda kuangalia namna bora ya kuboresha mazingira hayo kabla ya michezo mingine.

Mshindi wa riadha upande wa wanaume katika umbali wa mita 3000, 1500,800 na 400 Dogratius Sule kutoka kanda ya nyanda za juu kusini, amesema matarajio yake ni kufanya vizuri katika mashindano mbali mbali atakayoshiriki kwa ajili ya kupata fursa za kimataifa.

Mshindi kwa upande wa wanawake kutoka nyanda za juu kusini Denaa Gidashe,aliyeshinda katika nafasi ya kwanza katika mbio za mita 5000 na 3000, huku katika mbio za mita 1500, akishika nafasi ya tatu, amesema ni wakati muafaka kwa wanamichezo kutambua kuwa michezo wanayoshiriki ni ajira kama ajira zingine na kuwataka wazingatie miiko ya michezo wanayoshiriki.