May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri ataka usimamizi thabiti miradi ya shule

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKURUGENZI wa halmashauri zote nchini wametakiwa kuhakikisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule inayoendelea sasa katika halmashauri zao inasimamiwa ipasavyo ili ikamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratias Ndejembi alipokuwa akihutubia maelfu ya wanamichezo na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika wa uwanja wa shule ya sekondari ya wavulana Tabora.

Alisema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka mabilioni ya fedha katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ikiwemo kuboresha miundombinu iliyochakaa.

Alisisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kusimamiwa ipasavyo ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kuboreshwa miundombinu ya shule zote ili kuwajengea watoto mazingira mazuri ya kusomea na kuinua kiwango cha elimu nchini.

Ndejembi alibainisha kuwa mbali na ujenzi wa miundombinu katika shule za kidato cha 1-4 na kidato cha 5-6 pia itaboresha miundombinu ya michezo katika shule maalumu 56 zilizotengwa kwa ajili ya kuinua vipaji.

‘Kama alivyoelekeza Makamu wa Rais nasisitiza miundombinu ya shule zote ikamilike kwa wakati na iwe na ubora unaotakiwa, shule zote ziwe na viwanja vya michezo na mazingira yatunzwe vizuri’, alisema.    

Naibu Waziri aliongeza kuwa serikali imedhamiria kuwapandisha madaraja walimu wote wanaostahili katika mwaka ujao wa fedha hivyo akaelekeza Wakurugenzi kufanya uhakiki wa walimu wote waliokidhi vigezo na kuwasilisha majina Ofisi ya Rais TAMISEMI kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Pia aliwataka Wakurugenzi kuanza maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano ili watakaporipoti katika shule walizopangiwa waanze masomo mara moja pasipo changamoto yoyote.

Aidha ili maboresho ya miundombinu ya shule yalete tija aliwataka Maafisa Elimu wa ngazi zote kuhakikisha nidhamu kwa walimu na malezi bora kwa watoto vinaendelea kudumishwa katika shule zao.