May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashauri 99 ya kinidhamu yatolewa uamuzi Mahakamani

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, TABORA

TUME ya Mahakama na Utumishi nchini imepokea, kusikiliza na kutolea maamuzi jumla ya mashauri 99 ya kinidhamu kwa Watendaji wake kati ya mwezi Desemba 2015 na Desemba 2022.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Mahakama na Utumishi nchini alipokuwa akiongea na Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Watendaji Wakuu wa Mahakama. katika ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini hapa.

Alisema mashauri hayo yalihusu Mahakimu na Watendaji wa muhimili huo katika masuala ya kinidhamu baada ya kupitia katika kamati mbalimbali za kimaadili.

Alibainisha kuwa asilimia 33 ya watumishi waliobainika kuhusika moja kwa moja katika mashauri hayo walifukuzwa kazi, asilimia 38 walisimamishwa kwa manufaa ya umma, asilimia 13 walipewa onyo na asilimia 15 walirudishwa kazini.

Alifafanua kuwa viongozi wa kamati za maadili wamesaidia sana kuuheshimisha muhimili huo baada ya kuonekana tuhuma za kimaadili na kuzishughulikia ipasavyo, na katika hili hakuna mtumishi yeyote aliye juu ya sheria.

‘Ni muhimu sana kwa viongozi kujua changamoto zinazoikabili taasisi na kuzishughulikia kwa wakati ili jamii iendelea kuamini chombo chao cha utoaji haki’, alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alibainisha kuwa ukubwa wa eneo la kiutawala kama ulivyo Mkoa wa Tabora wakati mwingine linakuwa na changamoto kiutendaji zinazoweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu kwa mahakimu kumbe mtumishi anakuwa amezidiwa kutokana na ukubwa uliopo hivyo kushindwa kufikisha huduma kwa wakati.

Alisisitiza kuwa maboresho yanayoendelea sasa katika Mahakama zote nchini yatasaidia sana kupunguza changamoto za kiutendaji ikiwemo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Awali akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Katibu Tawala wa Mkoa Dkt John Mboya alipongeza kazi nzuri inayofanywa na mhimili  huo kwa wananchi na kubainisha kuwa elimu zaidi inahitajika ili wananchi waelewa umuhimu chombo hicho.

Dkt Mboya alibainisha kuwa mkutano huo umeongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya kimahakama na kamati zimepata elimu ya kutosha ya namna bora ya kupokea malalamiko ya wananchi.