January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazazi watakiwa kutowatenga watoto

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

WAZAZI wameaswa kuacha kuwalaza kwenye vitanda vyao watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi miwili kwani kufanya hivyo ni kuwakosesha haki yao ya msingi ya kunyonya.

Afisa kutoka taasisi ya chakula na lishe (TFNC), Neema Joshua ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa mada kwa waandishi wa habari katika wiki ya unyonyeshaji iliyoanza Agosti Mosi na kuhitimishwa Agosti 7 mwaka huu.

Amesema siku hizi kuna baadhi ya akina mama wamekuwa wakinunua vitanda vya watoto na kuwalaza peke yao jambo ambalo si sahihi kwani kitendo hicho kinamfanya mtoto kukosa haki ya kunyonya kutokana na wataalamu wa afya kushauri mtoto kunyonya mara kwa mara mchana na usiku .

“Siku hizi kuna vitanda vya watoto, unakuta mama amemlaza mtoto kitanda cha peke yake tena usiku halafu yeye analala na baba, hata kama unalala na baba hakikisha na mtoto mnalala naye ili anyonye kila inapohitajika,” amesema Neema.

Waandishi wa habari wakiwa katika semina ya Wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika jijini Dodoma katika ofisi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Picha na Joyce Kasiki )

Akizungumzia kuhusu ulishaji wa watoto wenye umri wa miezi sifuri hadi miezi sita, Afisa kutoka TFNC, Mary Kibona amesema, katika kipindi hicho mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee kwani yana virutubisho vyote muhimu na yanakidhi mahitaji yake yote.

“Maziwa ya mama ndio chakula pekee na kinywaji pekee cha mtoto katika miezi sita ya mwanzo na kinamsaidia kupata mahitaji yake msingi katika ukuaji wake,” amesema Kibona

Kuhusu ulishaji wa watoto wa miezi 6 hadi 24 (miaka miwili), Afisa kutoka TFNC, Valeria Millinga amewahimiza wazazi kuwapa watoto vyakula vya aina mbalimbali ili kumpatia mtoto hamu ya kula badala ya kumpa chakula cha aina moja kila siku.

Pia amesema, mtoto anapaswa kulishwa chakula kwa kipimo maalum na kumlisha kwa upendo na kwa kubuni mbinu za kumlisha mtoto kwa upendo na utulivu badala ya kumkaba na kumbana pua kwani njia hiyo siyo sahihi na inaweza kusababisha athari kwa mtoto .